 |
| Papa Francis |
 |
| Papa Francis akiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta |
Nairobi, Kenya
KIONGOZI wa Kanisa la Katoliki Duniani, Papa Francis, amewasili
nchini Kenya juzi jioni huku akitoa baraka kwa nchi hiyo kwa lugha ya
Kiswahili.
Baada ya hotuba yake, Papa Francis, alimaliza kwa kusema “Mungu
Ibariki Kenya” jambo lililowafanya watu waliokuwa katika ukumbi wa Ikulu
ya Nairobi kulipuka kwa furaha.
Katika ziara yake hiyo ya ya siku tatu nchini Kenya, alipokewa na
mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, ambapo moja ya mambo ya kukumbukwa ni
ujumbe alioutoa kwa Kiswahili akilibariki taifa hilo baada ya
kulihutubia taifa Ikulu jijini Nairobi.
Pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa amani, maridhiano,
kusameheana na uponyaji katika taifa hilo lililogawanyika kwa misingi ya
ukabila.
Baada ya mazungumzo yao Ikulu, Rais Kenyatta akagusia kwamba jana ni
siku ya maombi ya taifa la Kenya na baadaye akamkaribisha Papa Francis
kulihutubia taifa.
Papa alianza kutoa hotuba akishukuru kwa makaribisho mema kwenye ziara yake ya kwanza Afrika.
Kuhusu matarajio ya ziara yake, Papa alisema Kenya ina vijana wengi,
na hivyo katika siku zake za kuwa humo anasubiri kwa hamu kubwa kukutana
na kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za
usoni.
Aidha alisema Kenya ni taifa changa, linalokua na lenye jamii mseto
na ambalo limekuwa likitekeleza jukumu muhimu katika kanda hii na
kupitia changamoto nyingi katika uundaji wa demokrasia kama ilivyo kwa
mataifa mengi Afrika.
Akihimiza amani na maridhiano Papa Francis alisema: “Jamii zetu
zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko ya kikabila, kidini au kiuchumi,
binadamu wote wenye nia njema huitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha
na uponyaji.
“Yote ni katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha
utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema
linapaswa kuwa kipaumbele kikuu.”
Aidha alisema kwamba historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na
ugaidi huchochewa na kuogopana na kutoaminiana ambako husababishwa na
umaskini na kupoteza matumaini.
“Vita dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinapaswa kuendeshwa na
wanaume na wanawake wanaoamini katika kushadadia, maadili makuu ya
kidini na kisiasa ambayo yalisababisha kuasisiwa kwa taifa,” alisema.
Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Papa Francis alisema:
“Kenya imebarikiwa si tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa,
misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili.
“Wakenya wamethamini zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa
utamaduni wao wa kuhifadhi mazingira. Mgogoro wa kimazingira unaoikumba
dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano kati ya binadamu na
maumbile.”
Alihimiza taifa kuwajali masikini, ndoto za vijana, na kugawana vyema
maliasili na nguvu kazi ambazo Mungu ameibariki Kenya na ameahidi
kuendelea kwa juhudi za Kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na
kusaidia jamii, kutoa mchango katika hilo.
Akimalizia hotuba yake kabla ya kuondoka katika ukumbi wa Ikulu,
baada ya kusalimiana na baadhi ya wageni waalikwa alisema: “Nawashukuru
tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na familia zenu, na watu wote wa
Kenya, ziwe baraka tele za Mwenyezi Mungu.” Kisha akamalizia kwa
Kiswahili akisema: “Mungu Ibariki Kenya”.
Baada ya hotuba hiyo, Papa alikaribishwa katika dhifa ya kitaifa
iliyofanyika katika hema kubwa la mviringo eneo la Milimani, Nairobi,
ambako ni makazi ya rais na ofisi yake.
Awali ndege iliyombeba Papa ya Shirika la Ndege la Italia, Alitalia,
ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa
10. 33 jioni.
Viongozi wa Kanisa la Katoliki nchini humo, wanasiasa na mabalozi wakiongozwa na Rais Kenyatta walionekana wamejiandaa kumlaki.
Waandishi wa habari walioambatana na Papa walitangulia dakika 17
baadaye, kabla ya yeye mwenyewe kuchomoza kutoka katika ndege hiyo
dakika mbili zilizofuata.
Papa alilakiwa kwa shangwe na nderemo huku kwaya ya kumkaribisha
ikitumbuiza, na alianza kusalimiana na Rais Kenyatta kabla ya kutembezwa
kutambulishwa na kushuhudia vikundi mbalimbali vya utamaduni.
Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Serikali ya Kenya, Papa Francis
akiwa JKIA aliandika maneno haya: “Na maombi na shukrani kwa kuwatunza
wasafiri.”
Papa baada ya kupokewa kwa heshima zote za kitaifa uwanjani hapo,
msafara ulianza kuelekea Ikulu ya Nairobi ukipita mitaani, ambako maelfu
ya Wakenya walijipanga pembeni mwa barabara kumsalimia, huku wengine
wakipeperusha bendera na mabango ya kumkaribisha yakiwamo yenye picha
yake.
Alipokewa Ikulu na Rais Kenyatta, ambako wimbo wa taifa ulipigwa
kabla ya mizinga 21 kupigwa kwa heshima yake kama mkuu wa taifa la
Vatican.
Baadaye Papa Francis alikagua gwaride la heshima kabla ya kwenda
kuonana na Rais Kenyatta na baadhi ya wageni waalikwa na baadaye
kulihutubuia taifa akiwa Ikulu
Rais Kenyatta pia alimtambulisha Papa kwa wajumbe wa baraza lake la
mawaziri akiwamo naibu wake William Ruto kabla ya dhifa ya kitaifa
aliyomwandalia.
Kabla ya mazungumzo Ikulu, Papa Francis, ambaye anajulikana kwa
uhimizaji, utunzaji wa mazingira, pia alipanda mti akisaidiwa na Rais
Kenyatta.
Mbele ya hema kulikuwa na kiti ambacho Papa alikaa pembeni ya Rais Kenyatta.
Wakati Papa akitarajia kukutana na watu wa kawaida wakati wa ziara
yake Kangemi kesho na kukutana na vijana huko Kasarani, mkutano wake wa
kwanza ulikuwa jana na tabaka la watawala na vigogo wa Kenya.
Marais wastaafu Daniel arap Moi na Mwai Kibaki, Naibu Rais William
Ruto na Mke wa Rais, Margaret Kenyatta walikuwapo viti vya mbele wakati
wa dhifa ya taifa wakiwa mkabala na Papa na Rais Kenyatta.
Pembeni yao walikuwepo maspika Justin Muturi na Ekwee Ethuro na wake
zao. Wengine katika mstari wa mbele walikuwepo Jaji Mkuu Willy Mutunga,
Waziri wa Mambo ya Ndani Joseph Nkaissery, Makamu wa Rais wa zamani
Moody Awoli
Wengine ni Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Wachache katika Seneti Moses
Wetang’ula, viongozi wa muungano wa Cord, Kalonzo Musyoka na Raila
Odinga na mkewe Ida pia walitarajia kuhudhuria dhifa hiyo.
Majaji wa mahakama ya juu, wabunge, majaji na wengineo pia walitarajia kuwapo jana usiku.
Papa leo asubuhi anatarajia kuongoza ibada itakayohudhuriwa na watu milioni 1.4 kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Nairobi.
Awali kutokana na shauku ya kuwasili kwake nchini Kenya, mapema jana
Papa Francis alirusha ujumbe wa baraka kwa Wakenya kwenye mtandao wa
jamii.
Katika ujumbe wake alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter,
@Pontifex the Papa aliandika kwa Kiswahili na Kiingereza maneno: “Mungu
Ibariki Kenya!”
Aliutuma ujumbe huo jana mchana wakati akiwa safarini kutoka Rome, Italia kuelekea Nairobi.
Papa pia atazuru Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ambayo imekumbwa na machafuko baina ya Wakristo na Waislamu.
“Naenda nikiwa na furaha ya kuonana na Wakenya, Waganda na ndugu zetu
katika Afrika ya Kati,” aliwaambia waandishi wa habari katika ndege
yake.
Pia alipuuza wasiwasi wa usalama wake kwa kutania: “Ninaogopa zaidi mbu kuliko vita.”
Nairobi, linakuwa jiji la kwanza la Afrika, ambalo Papa huyo mwenye
umri wa miaka 78 ametua tangu akabidhiwe uongozi wa kanisa miaka miwili
iliyopita.
Anaitumia ziara yake ya 11 nje ya makao makuu ya kanisa hilo, Vatican
kutoa jumla ya hotuba 19 kuhusu amani, haki za kijamii, utunzaji wa
mazingira na majadiliano ya imani tofauti nchini Kenya, Uganda na CAR.
Wakati huo huo, muungano wa watu wasiotambua uwepo wa Mungu,
umewasilisha malalamiko yao mahakamani kupinga hatua ya Serikali ya
Kenya kuitangaza Alhamisi kuwa siku ya mapumziko ya taifa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa muungano huo, Harrison Mumia, wanaitaka
mahakama itupilie mbali tangazo lililochapishwa katika gazeti la
Serikali kuwa Alhamisi itakuwa siku ya mapumziko.
Juzi Rais Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa Novemba 26 (jana) iwe
mapumziko ya taifa kwa kuomba na kumwabudu Mungu wakati wa ziara ya
Papa.