Tafuta katika Blogu Hii

Jumanne, 3 Januari 2017

Mashekhe 18 washikiliwa na polisi-Uganda

                                                                    

Idadi ya mashekhe waliouawa inasadikiwa imefikia 17, na kati yao wanne ni mashekhe maarufu nchini Uganda.
Mashekhe 18 wamekamatwa wiki iliyopita na polisi nchini Uganda kufuatia wimbi la mauaji ya kushangaza ya mashekhe nchini humo.
Kwa mujibu wa duru za habari jijini Kampala kuna makundi mawili yanayo gongana katika misikiti miwili mikubwa, mmoja uko eneo la Nakasero na mwingine mjini Kampala.
Akiongea na VOA, Sheikh mmoja kwa sharti kutotajwa jina amesema kwamba Baraza Kuu la Umoja wa Waislamu Uganda limegawanyika katika makundi matatu. Lakini makundi mawili ambayo yaliamua kujitoa katika baraza hilo hayatambuliwi na serikali.
“Kundi ambalo linatambuliwa na serikali ni lile ambalo ofisi zake ziko Old Kampala, mengine ambayo yako Kibuli na Nakasero hayatambuliwi,” alifafanua.
Pande hizo zimehasimiana na zimeendelea kushutumiana na inasemekana zimeshindwa kufikiasuluhu. Mpaka sasa jumla ya mashekhe waliotiwa kizuizini ni 45.
Lakini wachambuzi wa mambo ya dini wanasema tatizo lililopo linafungamana na ushindani wa makundi haya mawili ambayo sasa imechukua sura mpya baada ya baadhi ya viongozi wa dini kuuwawa.
“Kinachotokea hivi sasa kila wakati sheikh anapouliwa kutoka upande mmoja, pande nyingine zinanyoosha vidole kulaumu kundi jingine na hivyo polisi huenda na kuwakamata watu hao,” alielezea kwa undani.
Mtu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema hadi hivi sasa idadi ya masheikh waliouwawa imefikia 17, na kati yao wanne ni masheikh maarufu nchini Uganda.
Lakini habari tulizopokea kutoka katika duru za kiislamu nchini Uganda zinasema imekuwa vigumu kwa Baraza Kuu la Umoja wa Waislam Uganda kusuluhisha mgogoro huu kutokana na kugawanyika kwa chombo hicho katika makundi matatu.
“Baraza limegawanyika na kumekuwa na pande ambazo zinavutana,” alisema mtoaji habari kwa sharti jina lake lisitajwe.
Lakini katika juhudi za kutafuta suluhu kati ya makundi haya bunge la Uganda lilijaribu kuingilia kati suala hili mara tu pale mauaji yalipoanza na kuiomba polisi kuchukua hatua mara moja.
Moja ya kero za wabunge waliokuwa wanajadili mada hii bungeni ilikuwa kitendo cha polisi kuvamia misikiti na kuifunga mashariki mwa Uganda, kitu ambacho kilikuwa kinaingilia uhuru wa kuabudu, alisema mmoja wa wabunge hao.
Lakini kuna pia taarifa kwamba kukamatwa kwa mashekhe kunatokana na kifo cha meja Sulaiman Kigundu aliyeuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Dereva wake pia aliuwawa katika tukio hilo.
Chanzo cha habari hii kinaeleza kuwa mashekhe hawa wanashukiwa kuwa wamehusika na kifo hicho.
“Tunaelezwa na jeshi la polisi kwamba wameshikiliwa ili kusaidia katika upelelezi wa vifo hivyo,” alisema moja wa waumini mjini Kampala.
Kigundu alikuwa mmoja wa wapiganaji wa chama cha Allied Demokratic Forces ambaye serikali ya Uganda ilimpa msamaha ili ajisalimishe.
ADF ni kundi la waasi kinachoipinga serikali ya Uganda na kinatambulika kama kundi la kigaidi.

Askofu aliyewapatia silaha Wapalestina afariki

                                                                                 

Aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa katoliki mjini Jerusalem ambaye alipatikana na hatia ya kuwapelekea silaha wapiganaji wa Palestina amefariki akiwa na umri wa miaka 94.
Hilarion Capucci alihudumia kifungo cha miaka 12 jela nchini Israel kabla ya Vatican kuingilia kati na kusaidia kumwachilia huru.
Alikuwa na historia ya uanaharakati unaohusishwa na mgogoro unaondelea mashariki ya kati.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alituma risala za rambi rambi akimtaja kuwa alikuwa mpiganiaji wa uhuru.
Vatican ilithibitisha kifo chake siku ya Jumatatu ,lakini haikusema kiini cha kifo hicho ama hata kutoa maelezo.
Capucci alizaliwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria Allepo mwaka 1922.
Alitawazwa kuwa kasisi wa kanisa la Allepo mwaka 1947 kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jerusalem.
Mwaka 1974, alikuwa akisafiri kutoka Beirut kuelekea Jerusalem ndani ya gari lililokuwa na nambari za mwanadiplomasia wakati liliposimamishwa na vikosi vya usalama vya Israel.
Ndani yake kulikuwa na bunduki nne aina ya Kalashnikov, bunduki nyengine mbili aina ya pistol , silaha na maguruneti yalionuia kupewa wanachama wa PLO.
Capucci alisisitiza kuwa ailazimishwa kusafirisha silaha hizo ,lakini mahakama ya Israel ilimpata na hatia ya kusafirisha silaha na kumuhukumu miaka 12 jela.
Aliachiliwa huru mwaka 1977 baada ya ombi la papa John Paul wa sita.
Capucci alisalia katika vyombo vya habari baada ya kuachiliwa kwake , akijaribu kuwa mpatanishi wa raia wa Marekani waliotekwa nchini Iran .
Ijapokuwa aliwakera baadhi ya mateka wa Marekani na matamshi yake wakati alipowatembelea ili kuangalia hali yao 1980, alihusika pakubwa katika usafirishaji wa miili minane ya wanahewa wa Marekani waliofariki katika jaribio la kuwaokoa wenzao.
Mwaka 1990, alisafiri hadi nchini Iraq chini ya uongozi wa Saddam Hussein ili kusaidia kuachiliwa huru kwa raia 68 wa Itali waliozuiliwa kuondoka nchini humo kufuatia uvamizi wa Kuwait.
Miaka 10 baadaye Capucci aliongoza ujumbe wa viongozi wa dini na wataalam nchini Iraq kwa umoja dhidi ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Mwaka 2010, alikuwa ndani ya meli ya Mavi Marmara wakati meli hiyo ya Uturuki ilioposimamishwa na makamanda wa Israel, iliposhiriki katika usafirishaji wa misaada ili kujaribu kukiuka kizuizi cha Ukanda wa Gaza.
Wanaharakati 10 wa Uturuki , mmoja wao akiwa raia wa Marekani mwenye uraia wa mataifa mawili ,waliuawa na makumi kujeruhiwa wakati ghasia zilipozuka baada ya makamanda hao kuingia katika meli hiyo,wakishuka kutoka kamba za helikopta.
Capucchi anasema kuwa uvamizi huo haukukubalika.

Jumatatu, 2 Januari 2017

Mwaka mpya na uongozi mpya Umoja wa Mataifa

                                                                          

Guterres ameahidi kufanya kazi na uongozi wa Trump ingawaje kumekuwepo na msuguano na atajaribu kushirikiana katika kuondoa "changamoto mbali mbali" ambazo Marekani na Umoja wa Mataifa zitakabiliana nazo siku za usoni.
Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres tayari ameshachukua madaraka ya juu katika taasisi ya dunia Jumapili, baada ya Ban Ki Moon kumaliza muda wake Desemba 31 saa sita usiku.
Guterres, ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Ureno na aliyekuwa kamishna wa idara ya Umoja wa Mataifa ya kuhudumia wakimbizi, ameiambia taasisi hiyo ya dunia katika hotuba yake kuwa suala la namna ya kuwasaidia watu waliokumbwa na migogoro na vita lina uzito mkubwa moyoni mwake.
Aliongeza kuwa wananchi wasio na hatia wanaendelea kukabiliwa na nguvu za kikatili, wanauawa na kujeruhiwa, wanatobanduliwa katika makazi yao na kutumbukizwa katika ufukara. Alilalamika kuwa hata mahospitali na misafara ya misaada haiko salama tena kutokana na vita.
Guterres amewataka wafanyakazi wenzake Umoja wa Mataifa "kukubaliana katika azimio moja la pamoja la mwaka mpya: Hebu basi tukubaliane kwamba amani ndiyo kitu cha kwanza."
"Hili lionekane kutoka kwenye mshikamano wetu na upendo wetu katika maisha yetu ya kila siku na mazungumzo na kuheshimiana katika migawanyiko yetu ya kisiasa," alisema.
Guterres ameahidi kuwa ni mwenye kuiunganisha dunia wakati rais mteuli wa Marekani, Donald Trump ameeleza wasi wasi wake kuwa Umoja wa Mataifa haina mashiko.
Hata hivyo Guterres ameahidi kufanya kazi na uongozi wa Trump ingawaje kumekuwa na msuguano na atajaribu kushirikiana katika kuondoa "changamoto mbali mbali" ambazo Marekani na Umoja wa Mataifa watakabiliana nazo siku za usoni.
Ban, ambaye amemaliza muda wake amewaambia wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika hotuba yake ya mwisho aliyoitoa Ijumaa "anajivuna sana" kufanya kazi nao kwa miaka kumi iliyopita.
Amewasihi waweke vipaumbele vyao na kuendelea kufuata malengo yao ya juu ya mambo ya maendeleo endelevu, kama vile mabadiliko ya tabia nchi, kuwawezesha wanawake, kuwawezesha vijana na mambo mengi mengineyo.

China kupiga marufuku biashra ya pembe za ndovu

Serikali ya China imetangaza kwamba itapiga marufuku biashara ya pembe za ndovu na viwanda vya kuchonga pembe hizo ifikapo mwisho wa mwaka 2017.
Baraza la mawaziri la China katika taarifa yake hapo Ijuma, limeeleza kwamba “ili kulinda vyema ndovu na njia bora ya kupambana na biashara haramu China itasitisha hatua baada ya hatua viwanda na uuzaji wa pembe kwa ajili ya biashara, ifikapo mwisho wa 2017.”
China imekua ikikabiliwa na shinikizo kutoka Jumuia ya Kiamtaifa kukomesha utumiaji wa bidhaa za pembe. Na mwezi Machi baada ya mkutano kati ya marais Barack Obama na Xi Jinping, serikali ya Bejing ilieleza kwamba itapanua marufuku ya pembe na bidhaa za pembe zlizoagiziwa kutoka nje kabla ya 1975.
"Haya ni mabadiliko makubwa kwa ndovu wa afrika", alisema Aili Kang, mkurugenzi wa kitengo cha Asia cha Tasisi ya kulinda Wanyamapori iliyoko New York. “Nina fahari kubwa kwa nchi yangu kuonesha uwongozi ambao utasaidia kuhakikisha kwamba ndovu wana uwezo hivi sasa ya kunusurika na kutotoweka duniani.”
Shirika la habari la China Xinhua linaeleza kwamba marufuku hiyo itasababisha kufungwa kwa viwanda 34 na vituo 143 vya bishara vilivyoidhinishwa.
Biahsra ya peme ilipigwa marufuku 1989 na mkataba wa kimataifa chiniya shirika la CITES. China ndio soko kuu la duniani la biashara ya pembe za ndovu.

Korea Kaskazini kutengeza kombora la masafa marefu

Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema kuwa taifa lake linakaribia awamu ya kutengeza kombora la masafara marefu ambalo lina uwezo wa kubeba bomu la nuklia.
Katika hotuba ya kuukaribisha mwaka mpya iliopeperushwa hewani katika runinga ya taifa Bw Kim amesema kuwa Korea Kaskazini imeimarika kama taifa lenye uwezo wa kinyuklia mwaka 2016.
Pyongyang imefanya majaribio mawili ya kombora la kinyuklia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikiwa ni mojawapo ya majaribio yake makubwa kufikia sasa.
Hatua hiyo ilizua shutuma mbalimbali na kuvutia vikwazo vya kimataifa .
Haijulikani taifa hilo imekaribia kivipi kutengeza kombora la Kinyuklia ambalo linaweza kurushwa na kufika Marekani.

Yahya Jammeh afungia kituo kinachomkosoa

Mamlaka nchini Gambia imekifunga kituo kimoja cha habari ambacho kimekuwa kikimkosoa rais wa taifa hilo Yahya Jammeh.
Maafisa wa Ujasusi waliagiza kituo cha habari cha Teranga FM kufungwa bila ya kutoa sababu ,alisema Emil Touray mkuu wa vyombo vya habari nchini humo.
Hii ni ishara ya kwanza ya vita dhidi ya vyombo vya habari tangu bwana Jammeh kukataa kushindwa katika uchaguzi wa Disemba mosi.
Bwana Jammeh alichukua mamlaka katika mapinduzi ya serikali mwaka 19194.
Awali alikuwa amekubali kushindwa na mfanyibiashara Adama Barrow, lakini akaenda mahakamani ili kupinga matokeo hayo,akisema uchaguzi hu ulikumbwa na udanganyifu.
Tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru.

Trump na Ngueso kuijadili Libya

Rais Denis Sassou Ngueso wa Jamhuri ya Kongo atakutana na rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kuujadili mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Libya, pamoja na masuala mengine yanayolihusu bara la Afrika. Msemaji wa Nguesso, Thierry Moungalla, amethibitisha  taarifa hiyo kupitia mtandao wa Twitter. Wawakilishi wa Trump, anayetarajiwa kuanza rasmi majukumu yake Januari 20, hawakuwa tayari kuthibitisha mara moja juu ya kuwepo kwa mkutano huo. Libya imekuwa ikikabiliwa na mgogoro wa kisiasa kufuatia pande mbili za kiserikali nchini humo kuhasimiana huku makundi mengine yaliyo na silaha nayo pia yakipambana kuwania madaraka. Mapema mwezi huu, Umoja wa Mataifa ulielezea juu ya mgogoro wa kibinadamu nchini Libya, ambao unazidi kuyafanya mapambano dhidi ya wahamiaji haramu kuwa magumu.