Tafuta katika Blogu Hii

Jumatano, 30 Novemba 2016

Njama za mauaji alizoepuka Fidel Castro

                      Shirika la kijasusi nchini Marekani CIA na watu waliotoroka Cuba wakati wa uongozi wa Castro walitumia nusu ya karne moja kufanya njama za kumuua kiongozi ambaye taifa lake lina athari kubwa kwa Marekani, kulingana na balozi wa Marekani nchini Cuba Wayne Smith.
Wakati mmoja kiongozi huyo wa Cuba alinukuliwa akisema, iwapo kuepuka majaribio ya mauaji kungekuwa miongoni mwa michezo ya Olimpiki ningejishindia medali ya dhahabu.
Hatahivyo baadhi ya njama hizo hazikutekelezwa ,kulingana na aliyekuwa mlinzi wa zamani wa Fidel Castro, Fabian Escalante.
Stakhabadhi zilizofichuliwa wakati wa utawala wa Bill Clinton zilionyesha kuwa CIA wakati mmoja walianza kuwafanyia utafiti konokono wa eneo la Carebean.
Njama, ilikuwa kutafuta konokono mmoja ambaye angemvutia Castro anayependa sana kuogelea na kumjaza vilipuzi ndani yake kabla ya kumlipua Castro atakapomshika
Mpango mwengine ulikuwa ule wa kutengeza boya la kuogelea ambalo huvaliwa kama shati na ambalo lingetiwa ugonjwa mbaya wa ngozi ili kumuathiri kiongozi huyo.
Mipango yote hiyo ilitupiliwa mbali.
Ajenti huyo alisikitika na akataka mpango mwengine ambao sio rahisi kuugundua,ripoti hiyo ilisema.
Mmoja ya wapenzi wa Castro wa zamani ,Marita Lorenz alisajiliwa.
Alipewa dawa zenye sumu ili kuweka katika kinywaji cha Castro.Lakini Castro aligundua jaribio hilo na anadaiwa kumpatia bunduki yake badala yake atumie kumuua.
''Huwezi kuniua. Hakuna anayeweza kuniua,"Bbi Lorenzo alisema Bw Castro alimwambia, alipokuwa anahojiwa na gazeti la New York daily.
Castro alidaiwa kutabasamu na kuendelea kuvuta sigara yake.''Nilijihisi nimetolewa pumzi kwa sababu alikuwa na uhakika juu yangu.Alinikumbatia na tukafanya mapenzi''.
Jaribio jingine lililokuwa maarufu dhidi ya maisha ya Castro ni lile la 2000, wakati ambapo mpango uliwekwa kuweka vilipuzi vingi katika jukwaa ambalo alitarajiwa kuhutubia nchini Panama.
Mpango huo ulitibuliwa na vikosi vya usalama vya Castro.
Watu wanne ikiwemo mtoro mmoja wa Cuba pamoja na ajenti wa CIA kwa jina Luis Posada walifungwa lakini baadaye wakaachiliwa.
Pia kulikuwa na mipango ya kumfanya Castro ambaye pia anajulikana '' The Beared'' aonekana kama chombo cha kukejeliwa badala ya kumuua.
Mpango mmoja ulikuwa kumwagia viatu vyake chumvi ya thallium wakati wa ziara yake ya ughaibuni kwa lengo kwamba anaposhika ndevu zake zingeweza kukatika.
Lakini mpango huo ulitibuliwa baada ya Castro kuahirisha ziara hiyo.Castro alichukua tahadhari ya hali ya juu ili kuwakwepa watu waliopanga mauaji yake.
Mwaka 1979 alipokuwa akielekea mjini New York ili kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa hakuweza kuwazuia wanahabari waliomuuliza iwapo alikuwa amevaa fulana ya ndani ambayo ina kinga dhidi ya risasi, alivua shati lake na kuwaonyesha kifua chake.
''Nimevaa fulana ya kawaida'',alisema.
Miongo kadhaa awali mwaka 1975, tume ya bunge la seneti nchini Marekani ilifichua maelezo ya njama nane dhidi ya maisha ya Castro kwa kutumia vifaa ambavyo tume hiyo inasema ''vinachosha akili''.
Njama moja iliopangwa na ambayo karibu ifaulu mara mbili ilikuwa ile ya kutuma dawa za sumu Cuba na kuwapeleka watu kumuua kiongozi huyo.
Ulikuwa wakati kama huo ambapo rais Kennedy, ambaye aliruhusu uvamizi wa kumuondoa madarakani rais Castro mwaka 1961 aliuawa, ambapo ajenti wa CIA alikuwa anatoa kalamu yenye sumu ilio na sindano kwa ajenti mmoja wa Cuba ili kumuua kiongozi huyo.

Mkurugenzi wa CIA amuonya Trump

                    Mkurugenzi wa shirika la kijasusi nchini Marekani CIA amemuonya rais mteule wa Marekani Donald Trump kwamba kusitisha makubaliano ya mpango wa nyuklia na Iran itakuwa ''hatari na upuuzi''.
Katika mahojiano na BBC ,John Brennan pia alimshauri rais huyo mpya kuwa na tahadhari kuhusu ahadi mpya za Urusi akiilaumu Moscow kwa mateso yanayoendelea nchini Syria.
Katika kampeni yake ,bw Trump alitishia kufutilia mbali mpango wa mnyuklia nchini Iran mbali na kuashiria kufanya kazi kwa karibu na Urusi.
                    Bw Brenan atajiuzulu mnamo mwezi Januari baada ya kuhudumia shirika hilo kwa kipindi cha miaka minne.
Katika mahojiano ya kwanza na vyombo vya habari vya Uingereza ,Brennan alitaja maswala kadhaa ambapo alisema kuwa utawala mpya unafaa kuzingatia kwa busara na heshima, ikiwemo lugha inayotumiwa kuhusu ugaidi, uhusiano na Urusi, mpango wa kinyuklia wa Iran na vile siri za shirika hilo hutekelezwa

Makampuni ya kigeni yalalamikia kodi

                         Baadhi ya makumpuni makubwa ya kigeni yaliyowekeza nchini Tanzania huenda yakafikiria kupunguza au kusitisha shughuli zake kwa sababu ya masharti magumu yanayowekwa dhidi ya makampuni hayo, ikiwemo kodi kubwa.
Kwa mujibu wa mahojiano yaliyofanywa na shirika la habari la Reuters pamoja na wakurugenzi wakuu wa makapuni ya kigeni yaliyowekeza nchini Tanzania, kiasi ya makampuni sita yanafikiria mipango mipya kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini, mawasiliano ya simu au usafirishaji kwa kutumia meli. Hiyo yote inatokana na juhudi zinazofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli kuubadili uchumi wa nchi hiyo.
Makampuni matatu yamesema huenda yakapunguza shughuli zake za uwekezaji kwenye taifa hilo la Afrika  Mashariki, huku makampuni mengine mawili yakisema yanafikiria kutanua zaidi shughuli zake katika nchi jirani na kampuni moja imesema inaandaa mchakato wa kujiondoa kabisa nchini Tanzania. Makampuni hayo yaliombwa kutotajwa majina kwa sababu ya umuhimu wa suala hili na kwa sababu mipango yao hiyo bado haijatangazwa hadharani.
Kampuni moja bado haijatoa msimamo wake jinsi ya kukabiliana na mageuzi hayo ya serikali ya Tanzania, huku makampuni matano yakisema kuwa mipango yao haikuathirika na mageuzi hayo, ikiwemo miradi miwili mikubwa, ule wa kiwanda cha kusindika gesi asilia-LNG wenye thamani ya Dola bilioni 30 na mradi wa kiwanda cha mbolea wenye thamani ya Dola bilioni 3.
                                    Tanzania na uwekezaji wa kigeni
Tanzania inategemea zaidi uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja, kuliko nchi nyingine za ukanda huo, kutokana na ukubwa wa uchumi wake. Mwaka uliopita nchi hiyo ilipokea zaidi ya Dola bilioni 1.5, kwenye uchumi ambao thamani yake ilikuwa chini ya Dola bilioni 45. Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Umoja wa Mataifa pamoja na Benki ya Dunia.
Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye amepewa jina la utani ''Tingatinga'' kutokana na miradi yake ya miundombinu na aina ya uongozi wake, alizindua mchakato wa mageuzi yake ya kiuchumi, baada ya kuchaguliwa kuiongoza nchi hiyo mwaka uliopita, akiahidi kuubadilisha uchumi wa nchi hiyo, kuondoa urasimu na rushwa pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi.
Mwaka huu serikali ya Magufuli iliongeza kodi katika utumaji wa fedha kwa kutumia simu za mkononi, mabenki, huduma za utalii na zile za usafirishaji wa mizigo. Kodi ya mapato kwa mwaka wa fedha 2014/2015 jumla ilikuwa Shilingi za Tanzania trillioni 9.8 ambazo ni sawa na Dola bilioni 4.5. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, serikali ina lengo la kukusanya kodi ya mapato zaidi ya trilioni 15.1, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Adolf Mkenda, amesema wameyasikia malalamiko yanayotolewa na milango iko wazi, lakini wanahakikisha kuwa kila mtu analipa kodi anayopaswa kulipa kwa kuzingatia haki. Amesema lazima kuwepo na mageuzi mapya ambayo ni magumu, ili kuufanya uchumi kuwa imara.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Richard Kayombo amesema ongezeko la kodi ya mapato lilihitajika kwa ajili ya kulipia miundombinu mipya nchini humo. Makampuni makubwa ya kigeni ambayo yamewekeza nchini Tanzania ni pamoja na yale ya nishati, uhandisi, mawasiliano ya simu, madini, na usafirishaji kwa kutumia meli.

Majivu ya Fidel Castro kusafirishwa Santiago

                                                                           

            Mwili wa Fidel Castro aliyefariki akiwa na umri wa miaka 90, Ijumaa wiki jana, ulichomwa moto kulingana na matakwa yake. Majivu yake yatapitishwa katika miji kadhaa nchini humo kwa siku tatu kwanzia leo, kabla ya kufikishwa mji wa Santiago ambako ndiko atazikwa siku ya Jumapili.
Mji wa Santiago unaojulikana kama chimbuko la ukomunisti wa Cuba, ndiko mapinduzi yaliyoongozwa na marehemu Castro yalianzia mnamo mwaka 1953 na akachukua urais mwaka 1959.  Hapo jana mamia ya maelfu ya waombolezaji walifika kumpa heshima za mwisho jijini Havana.
Rais wa Bolivia ni miongoni mwa waliohudhuria misa hiyo na alisema: "Fidel hajafa kwa sababu wanaopigania uhuru hawafariki. Huyo ni Fidel. Hajafa kwa kuwa mawazo hayafi hasa mawazo yanayoleta ukombozi. Fidel hajafa kwa kuwa mapigano hayajaisha hasa mapigano dhidi ya utengano. Fidel ni kama yuko hai kuliko zamani akiendeleza vita kuokoa makazi yetu ya pamoja".
Mazishi yake yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa wakiwemo marais Nicolas Maduro wa Venezuela, Daniel Ortega wa Nicaragua, Evo Morales wa Bolivia na Rafael Correa wa Equador, kando na wakuu wa nchi za Amerika ya kusini na mfalme wa zamani wa Uhispania Juan Carlos.
Uhusiano wa Cuba na Marekani
                                                                            



Fidel Castro alitawala Cuba kwa miaka 47, hadi alipojiuzulu mwaka 2006 kufuatia hali yake ya kiafya, na kumkabidhi nduguye Raul Castro. Tangu wakati huo hajajitokeza hadharani japo inaaminika alikuwa na wasiwasi na uhusiano ulioimarishwa mwaka 2014 kati ya nchi yake na hasimu wao wa jadi Marekani. Haijabainika ikiwa uhusiano huo utaendelea kuimarika baada ya Januari rais mteule wa Marekani Donald Trump atakapochukua rasmi urais.
Akitoa hotuba ya rambirambi jijini Havana, rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema "Cuba haikutafuta madini ya dhahabu, almasi au mafuta barani Afrika. Wacuba walitaka uhuru na mwisho wa unyanyasaji wa bara la Afrika kutumiwa kama kiwanja cha kuchezewa na nchi kubwakubwa huku watu wakiteseka".
Fidel Castro alipendwa na wengi duniani hasa Amerika ya kusini na Afrika, kwa kusimama dhidi ya Marekani, huku akizindua mipango ya elimu bure na huduma za afya bila malipo kando na kuwatuma madakitari wao katika mataifa mengine duniani kutoa misaada ya kiafya.
Lakini wengine walimshutumu kuwa kiongozi wa kiimla aliyevuruga uchumi kutokana na sera zake za usosholisti na kuwanyima wacuba haki za kibinadamu mfano uhuru wa kujieleza.

Jumamosi, 26 Novemba 2016

Timu ya Trump yagawanyika

Mgawanyiko katika timu ya mpito ya Rais-mteule Donald Trump kuhusu nani ateuliwe kuwa waziri wa mambo ya nje umeanza kutoka hadharani, na kusababisha nafasi hiyo kubaki wazi mpaka tofauti ndani ya timu hiyo zipatiwe ufumbuzi.
Makundi yanayopingana katika timu hiyo ya mpito yamegawanyika baina ya mgombea urais Mrepublican mwaka 2012 Mitt Romney na meya wa zamani wa jiji la New York Rudolph Giuliani.
Katika ujumbe wa Twitter Alhamisi, mshauri wa Trump, Kellyanne Conway alieleza hisia za upande unaompinga Romney. Conway alisema amepata "rundo" la maoni yenye wasiwasi ambayo yanahoji utiifu wa Romney ambaye alimshambulia sana Trump wakati wa kampeni za urais.
Wale wanaompinga Giuliani kama waziri wa mambo ya nje wanadai kuwa uhusiano wake mkubwa na makampuni ya nje huenda ukasababisha mvutano mkubwa katika vikao vya kumthibitisha katika baraza la seneti. Wanahoji pia endapo mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72 ana nguvu za kuweza kuwa anasafiri sana nje ya nchi kama kazi hiyo inavyohitaji.
Rais huyo mteule, ambaye amejizolea sasa sifa ya kugeuza misimamo yake, amewasifu wote Romney na Giuliani. Trump inasemekana aliwaambia wasaidizi wake kwamba Romney "anafanana" na nafasi hiyo lakini pia amekuwa akimsifu Giuliani pia.
Wengine ambao wanasemekana kufikiriwa katika nafasi hiyo ni pamoja jenerali mstaafu na mkurugenzi wa zamani wa CIA David Petraeus na Seneta Bob Corker wa Tennessee.

Mpiga picha Hamilton afariki

                     Mpiga picha Muingereza,mwenye utata David Hamilton, anayejulikana kwa kupiga picha za uchi za wana mitindo vijana, amepatikana amefariki nyumba kwake mjini Paris.
Taarifa za vyombo vya habari za Ufaransa zinasema dawa zilipatikana kandao ya maiti yake lakini kilichosababisha kifo chake bado hakija bainika.
Hadi kifo chake mpiga picha huyo mwenye umri wa miaka thamanini na tatu alikuwa akiendesha shughuli zake mjini Paris.
Alijizolea umaarufu wake miaka ya sitini. Hivi karibuni Hamilton,alituhumiwa kwa ubakaji na mwanahabari mmoja na kumekuwa na madai sawa na hayo kutoka kwa watu tofauti wanaoshughulika na kampuni za mamode hasa watoto.
Mapema wiki hii,Bwana huyo hata hivyo alitoa taarifa kukanusha vikali madai hayo na kutishia kuchukulia hatua za kisheria vyombo vya habari wanaoendeleza uvumi huo dhidi yake.

Moto mkali wawaka Israel,

              Takriban watu elfu 60 wameyakimbia makaazi yao  wakati ambapo polisi na vikosi vya wazimamoto wanapelekwa kwa wingi katika mji wa Haifa ambako inahofiwa kwamba moto huo mkali unaweza kuendelea kutokana na hali ya ukame inayoandamana  na upepo.  Watu kadhaa wamelazwa hospitali kutokana na madhara ya kuvuta moshi lakini hakuna taarifa zinazoashiria kuwa kuna watu walio katika hali mahututi.  Mamia ya nyumba za watu ziliharibiwa katika mkasa huo, Israel hapo jana ililazimika kuwaita maafisa wa jeshi wa akiba kuja kuungana na polisi wa nchi hiyo pamoja na wazima moto.  Vile vile maafisa hao waliitumia ndege maalum ya kupambana na moto mchango uliotolewa na jamii ya kimataifa.
Msemaji wa jeshi la polisi nchini Israel Micky Rosenfeld amesema shughuli za kuwahamisha watu zilifanyika jana usiku katika mji mdogo ulio karibu na jiji la Jerusalem baada ya nyumba kadhaa katika mji huo kushika moto.  Hadi kufikia sasa watu 12 wamekamatwa na wanatuhumiwa kuhusika na moto huo.  Viongozi wa Israel wanahisi kwamba moto huo umeanzishwa kwa
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelaumu vitendo vya uchochezi moingoni mwa Wapalestina kuwa ndio chanzo cha mashambulio hayo.  Moto huo ulianza siku tatu zilizopita katika eneo la jamii ya Neve Shalom karibu na mji wa Jerusalem eneo ambalo jamii za Kiarabu na Kiyahudi zinaishi pamoja.  Baadae moto ulizuka upande wa kaskazini katika eneo la Zichron Yaakov na kwengineko karibu na mji wa Jerusalem kabla ya moto mkubwa kuanza katika mji wa Haifa.  Nchi kadhaa zikiwemo Urusi, Ufaransa, Cyprus, Uturuki,Croatia,Ugiriki na Italia zimetuma misaada yao ya kupambana na moto huo.  katika hatua isiyo ya kawaida Wapalestina pia wamejiunga na wazima moto wa Israeli kusaidia kuuzima moto huo.
                   Maafa haya ni mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2010 wakati Israel ilikumbwa na moto mkubwa uliowahi kutokea katika historia, moto huo ulisababisha vifo vya watu 42 na wazima moto waliweza kuuzima baada ya siku nne pale ndege maalum ya kuzima moto ilipofika kutoka Marekani na kutokea wakati huo Israel imeimarisha vifaa na jeshi lake la kupambana na moto, imenunua ndege maalum za kuzima moto ambazo zina uwezo wa kumwaga maji mengi katika eneo husika.