Tafuta katika Blogu Hii

Ijumaa, 27 Novemba 2015

Papa Francis abariki kwa Kiswahili baada ya kutua Kenya.

Papa Francis
     
Papa Francis akiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta
     
Nairobi, Kenya
                          KIONGOZI wa Kanisa la Katoliki Duniani, Papa Francis, amewasili nchini Kenya juzi jioni huku akitoa baraka kwa nchi hiyo kwa lugha ya Kiswahili.
Baada ya hotuba yake, Papa Francis, alimaliza kwa kusema “Mungu Ibariki Kenya” jambo lililowafanya watu waliokuwa katika ukumbi wa Ikulu ya Nairobi kulipuka kwa furaha.
Katika ziara yake hiyo ya ya siku tatu nchini Kenya, alipokewa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, ambapo moja ya mambo ya kukumbukwa ni ujumbe alioutoa kwa Kiswahili akilibariki taifa hilo baada ya kulihutubia taifa Ikulu jijini Nairobi.
Pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa amani, maridhiano, kusameheana na uponyaji katika taifa hilo lililogawanyika kwa misingi ya ukabila.
                     Baada ya mazungumzo yao Ikulu, Rais Kenyatta akagusia kwamba jana ni siku ya maombi ya taifa la Kenya na baadaye akamkaribisha Papa Francis kulihutubia taifa.
Papa alianza kutoa hotuba akishukuru kwa makaribisho mema kwenye ziara yake ya kwanza Afrika.
Kuhusu matarajio ya ziara yake, Papa alisema Kenya ina vijana wengi, na hivyo katika siku zake za kuwa humo anasubiri kwa hamu kubwa kukutana na kuzungumza nao na kuwapa matumaini katika ndoto zao za siku za usoni.
Aidha alisema Kenya ni taifa changa, linalokua na lenye jamii mseto na ambalo limekuwa likitekeleza jukumu muhimu katika kanda hii na kupitia changamoto nyingi katika uundaji wa demokrasia kama ilivyo kwa mataifa mengi Afrika.
Akihimiza amani na maridhiano Papa Francis alisema: “Jamii zetu zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko ya kikabila, kidini au kiuchumi, binadamu wote wenye nia njema huitwa kufanyia kazi maridhiano, msamaha na uponyaji.
“Yote ni katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo kutenda mema linapaswa kuwa kipaumbele kikuu.”
Aidha alisema kwamba historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na ugaidi huchochewa na kuogopana na kutoaminiana ambako husababishwa na umaskini na kupoteza matumaini.
“Vita dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinapaswa kuendeshwa na wanaume na wanawake wanaoamini katika kushadadia, maadili makuu ya kidini na kisiasa ambayo yalisababisha kuasisiwa kwa taifa,” alisema.
Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Papa Francis alisema: “Kenya imebarikiwa si tu na umaridadi, katika milima, mito na maziwa, misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika utajiri wa maliasili.
                “Wakenya wamethamini zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa utamaduni wao wa kuhifadhi mazingira. Mgogoro wa kimazingira unaoikumba dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano kati ya binadamu na maumbile.”
Alihimiza taifa kuwajali masikini, ndoto za vijana, na kugawana vyema maliasili na nguvu kazi ambazo Mungu ameibariki Kenya na ameahidi kuendelea kwa juhudi za Kanisa Katoliki, kupitia kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika hilo.
Akimalizia hotuba yake kabla ya kuondoka katika ukumbi wa Ikulu, baada ya kusalimiana na baadhi ya wageni waalikwa alisema: “Nawashukuru tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na familia zenu, na watu wote wa Kenya, ziwe baraka tele za Mwenyezi Mungu.” Kisha akamalizia kwa Kiswahili akisema: “Mungu Ibariki Kenya”.
Baada ya hotuba hiyo, Papa alikaribishwa katika dhifa ya kitaifa iliyofanyika katika hema kubwa la mviringo eneo la Milimani, Nairobi, ambako ni makazi ya rais na ofisi yake.
                Awali ndege iliyombeba Papa ya Shirika la Ndege la Italia, Alitalia, ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa 10. 33 jioni.
Viongozi wa Kanisa la Katoliki nchini humo, wanasiasa na mabalozi wakiongozwa na Rais Kenyatta walionekana wamejiandaa kumlaki.
Waandishi wa habari walioambatana na Papa walitangulia dakika 17 baadaye, kabla ya yeye mwenyewe kuchomoza kutoka katika ndege hiyo dakika mbili zilizofuata.
Papa alilakiwa kwa shangwe na nderemo huku kwaya ya kumkaribisha ikitumbuiza, na alianza kusalimiana na Rais Kenyatta kabla ya kutembezwa kutambulishwa na kushuhudia vikundi mbalimbali vya utamaduni.
Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Serikali ya Kenya, Papa Francis akiwa JKIA aliandika maneno haya: “Na maombi na shukrani kwa kuwatunza wasafiri.”
Papa baada ya kupokewa kwa heshima zote za kitaifa uwanjani hapo, msafara ulianza kuelekea Ikulu ya Nairobi ukipita mitaani, ambako maelfu ya Wakenya walijipanga pembeni mwa barabara kumsalimia, huku wengine wakipeperusha bendera na mabango ya kumkaribisha yakiwamo yenye picha yake.
           

                Alipokewa Ikulu na Rais Kenyatta, ambako wimbo wa taifa ulipigwa kabla ya mizinga 21 kupigwa kwa heshima yake kama mkuu wa taifa la Vatican.
Baadaye Papa Francis alikagua gwaride la heshima kabla ya kwenda kuonana na Rais Kenyatta na baadhi ya wageni waalikwa na baadaye kulihutubuia taifa akiwa Ikulu
Rais Kenyatta pia alimtambulisha Papa kwa wajumbe wa baraza lake la mawaziri akiwamo naibu wake William Ruto kabla ya dhifa ya kitaifa aliyomwandalia.
Kabla ya mazungumzo Ikulu, Papa Francis, ambaye anajulikana kwa uhimizaji, utunzaji wa mazingira, pia alipanda mti akisaidiwa na Rais Kenyatta.
Mbele ya hema kulikuwa na kiti ambacho Papa alikaa pembeni ya Rais Kenyatta.
Wakati Papa akitarajia kukutana na watu wa kawaida wakati wa ziara yake Kangemi kesho na kukutana na vijana huko Kasarani, mkutano wake wa kwanza ulikuwa jana na tabaka la watawala na vigogo wa Kenya.
                   Marais wastaafu Daniel arap Moi na Mwai Kibaki, Naibu Rais William Ruto na Mke wa Rais, Margaret Kenyatta walikuwapo viti vya mbele wakati wa dhifa ya taifa wakiwa mkabala na Papa na Rais Kenyatta.                      
Pembeni yao walikuwepo maspika Justin Muturi na Ekwee Ethuro na wake zao. Wengine katika mstari wa mbele walikuwepo Jaji Mkuu Willy Mutunga, Waziri wa Mambo ya Ndani Joseph Nkaissery, Makamu wa Rais wa zamani Moody Awoli
Wengine ni Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Wachache katika Seneti Moses Wetang’ula, viongozi wa muungano wa Cord, Kalonzo Musyoka na Raila Odinga na mkewe Ida pia walitarajia kuhudhuria dhifa hiyo.
                            Majaji wa mahakama ya juu, wabunge, majaji na wengineo pia walitarajia kuwapo jana usiku.
Papa leo asubuhi anatarajia kuongoza ibada itakayohudhuriwa na watu milioni 1.4 kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Nairobi.
Awali kutokana na shauku ya kuwasili kwake nchini Kenya, mapema jana Papa Francis alirusha ujumbe wa baraka kwa Wakenya kwenye mtandao wa jamii.
                        Katika ujumbe wake alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, @Pontifex the Papa aliandika kwa Kiswahili na Kiingereza maneno: “Mungu Ibariki Kenya!”
Aliutuma ujumbe huo jana mchana wakati akiwa safarini kutoka Rome, Italia kuelekea Nairobi.
Papa pia atazuru Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ambayo imekumbwa na machafuko baina ya Wakristo na Waislamu.
“Naenda nikiwa na furaha ya kuonana na Wakenya, Waganda na ndugu zetu katika Afrika ya Kati,” aliwaambia waandishi wa habari katika ndege yake.
Pia alipuuza wasiwasi wa usalama wake kwa kutania: “Ninaogopa zaidi mbu kuliko vita.”
Nairobi, linakuwa jiji la kwanza la Afrika, ambalo Papa huyo mwenye umri wa miaka 78 ametua tangu akabidhiwe uongozi wa kanisa miaka miwili iliyopita.
Anaitumia ziara yake ya 11 nje ya makao makuu ya kanisa hilo, Vatican kutoa jumla ya hotuba 19 kuhusu amani, haki za kijamii, utunzaji wa mazingira na majadiliano ya imani tofauti nchini Kenya, Uganda na CAR.
                           Wakati huo huo, muungano wa watu wasiotambua uwepo wa Mungu, umewasilisha malalamiko yao mahakamani kupinga hatua ya Serikali ya Kenya kuitangaza Alhamisi  kuwa siku ya mapumziko ya taifa.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa muungano huo, Harrison Mumia, wanaitaka mahakama itupilie mbali tangazo lililochapishwa katika gazeti la Serikali kuwa Alhamisi itakuwa siku ya mapumziko.
Juzi Rais Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa Novemba 26 (jana) iwe mapumziko ya taifa kwa kuomba na kumwabudu Mungu wakati wa ziara ya Papa.

Jumatatu, 23 Novemba 2015

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA, 20 NOVEMBA 2015

 
Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo. Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi huu.

Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.

Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu mbili:


·          Kwanza, ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
·          Pili, nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki. Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka Wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani pia watafanya hivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na utulivu mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga kura. Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa, na hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.
Wale waliotarajia kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara nyingine tena tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa cha Amani katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya nchi yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.
Aidha, napenda niungane na ninyi pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa pamoja na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi. 
Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua za awali za kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa Spika;
          Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu wa nchi yetu walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi yetu. Natambua mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga misingi imara wa umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na kuijenga misingi yake. Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua na kuimarisha misingi ya uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao. Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.
Mhishimiwa Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja, tumeshindana katika kampeni tukiwa wamoja, na tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi za Umoja na Amani. Hatutakuwa na simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga umoja na amani yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila, vyama au ukanda.
Mheshimiwa Spika;
       Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza kwa kulalamikiwa sana na wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni pamoja na:
·          Rushwa - Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa wananchi.
·          TAMISEMI - Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k.;
·          Ardhi – Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;
·          Bandari - Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;
·          Maji – Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji kupatikana mbali na makazi, n.k.;
·          TRA - Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara wakubwa;
·          TANESCO - Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;
·          Maliasili na Utalii - Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;
·          Huduma za Afya (Hospitali) - Huduma kuwa mbali na wahitaji, Ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, n.k.;
·          Uhamiaji na Ajira - Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi nchini kwa wageni, Kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, n.k.;
·          Elimu - Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;
·          Polisi - Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari, Ukosefu wa nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;
·          Zimamoto – Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea kazi kama maji, n.k.;
·          Mizani – kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;
·          Mahakama - Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa kesi. Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.
·          Madini – Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia, n.k;
·          Kilimo na Mifugo – Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la masoko, Kukopwa mazao ya wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa Maghala, Mabwawa, Malambo, Majosho, n.k.;
·          Uvuvi – Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi hususan viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa bahari;
·          Reli – Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa reli, upungufu wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara, n.k.;
·          ATC – Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa mishahara ila ndege ni moja (1);
·          Makundi Maalum – Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa;
·          Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo – Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, Haki na maslahi yao, n.k.;
Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue na mshirikiane na Serikali na wadau wengine tuzitatue haraka.
Pamoja na kero hizo tutashughulikia pia mambo yafuatayo.
Kuimarisha Muungano
Mheshimiwa Spika;
Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani. Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu.
Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.
Serikali nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuendelea kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.
Kuimarisha Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaheshimu na kuendeleza utamaduni mzuri uliojengeka nchini wa kuheshimu mihimili ya dola. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata fedha za kutosha kuendesha shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Kwa upande wa Bunge, tutahakikisha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinapatikana kwa wakati ili Waheshimiwa Wabunge mkashirikiane na wananchi wenu kusukuma maendeleo. Kwa upande wa Mahakama, tutalipa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa Mahakama kwa kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, kuongeza kasi ya utoaji haki na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama zetu.
Mchakato wa Katiba
Mheshimiwa Spika;
Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba. 
Uchumi na Matarajio ya Wananchi
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kukiwa na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika Awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na kukua wastani wa asilimia 7. Katika kipindi hicho fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa. Hii ni kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali za Awamu zilizopita za kujenga miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, uimarishaji wa bandari, uimarishaji wa reli, na ukuzaji wa sekta za mawasiliano ya simu na mitandao, ukuzaji na uongezaji wa uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme.
Napenda kuwahakikishia kuwa tutaendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu mipya na kuiimarisha iliyopo ili kuvutia na kushawishi wawekezaji wa ndani na wa nje.
Mheshimiwa Spika;
Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa ahadi tulizowaahidi Watanzania ni kuendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya; barabara ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na upanuaji wa barabara za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga flyovers, barabara za pete (ring roads), n.k. Uboreshaji wa barabara na njia nyingine za uchukuzi na usafirishaji kuingia na kutoka Dar es Salaam ni muhimu sana kwa sababu bandari ya Dar es salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika;
Katika jitihada hizo hizo za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi Serikali ya Awamu ya Tano, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge). Reli ambazo tunakusudia zianze kujengwa ni:
·          Dar es Salaam – Tabora – Kigoma/Mwanza
·          Uvinza – Msongati (Burundi) na Isaka – Kigali (Rwanda)
·          Mtwara – Songea – Mbamba Bay na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga;
·          Tanga – Arusha – Musoma
·          Kaliua – Mpanda – Karema
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu pia imejaliwa kuwa na madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi asilia umeongeza matumaini ya watu wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi katika miaka ijayo. Serikali itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo. Aidha, napenda kuipongeza kwa dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Bunge la 10 kwa kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi yaani The Oil and Gas Revenues Management Act, 2015. Serikali yangu itasimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini mkubwa.
Ujenzi wa Viwanda
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda. Natambua kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Hatuna njia nyingine kama kweli tunataka kujenga msingi wa uchumi endelevu katika nchi yetu utakaopaisha uchumi na maisha ya watu wetu. Dira ya Maendeleo ya 2025 inatutaka tuwe nchi ya watu wenye kipato cha kati. Tunaweza tukafika huko, na dalili zipo, lakini pia tunaweza tukafika huko kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia wa mambo ni tofauti. Utofauti ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha kwamba sisi ni nchi ya kipato cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha ya watu wengi hazifanani na takwimu hizo. Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda.
Mheshimiwa Spika;
Tutahakikisha suala la viwanda linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa. Matarajio yangu ni kuwa Bunge lako Tukufu litatuunga mkono mimi na Serikali nitakayoiunda katika kufikia lengo hili.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema wakati wa Kampeni, na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda vilivyopo na kuhakikisha vinafanya kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa viwanda vilivyokuwa vya umma kwa makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka wafanye hivyo mapema. Na hapa nataka nisisitize wito wangu huo kwao. Najua huko nyuma ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya aina hiyo umekuwa ukilegalega na watu wamejifanyia mambo watakavyo. Wapo walioacha kabisa uzalishaji na kufumua hata mitambo ya uzalishaji. Mimi niliahidi, na nataka niseme hapa kwa wazi kabisa, kwamba wale waliobinafsishiwa viwanda hivyo waanze kazi, waanze kazi mara moja. Wakishindwa basi tutavitwaa viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na kuwapa watu wengine wenye nia ya kuviendeleza. Hatuwezi kuwa na watu wanajiita wawekezaji tunawapa viwanda vyetu halafu wanaviatamia tu. Mimi hilo sitalikubali na wala sitalivumilia. Nimeielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanza kushughulikia suala hili mara moja. Naomba Bunge lako lituunge mkono.
Mheshimiwa Spika;
Njia ya pili ya kuendeleza viwanda ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu ya kufanya hivyo tayari ipo na baada ya muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo watu wanaotaka kuwekeza Tanzania sasa, katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka ya nyuma kidogo, lakini wakati mwingine sisi humu humu – tukiwemo sisi viongozi kwa kushirikiana na wafanyabiashara matapeli na laghai – tumehujumu mipango na shauku ya wawekezaji wa nanma hiyo. Pamoja na shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea vikwazo na kuwapiga vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi jirani. Sisi katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa usumbufu na urasimu wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji wa Serikali watakaokwamisha jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda hapa nchini hatutawavumilia.   
Mheshimiwa Spika;
Ni viwanda vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura ya kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani, hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini – na maliasili nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana. Viwanda vya aina hii vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja, na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) – yaani bidhaa kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi vitakuwa na uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. Viwanda hivi vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje. Yote mawili yakitokea, yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje, itatuongezea akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na kuendeleza mipango mingine kwa ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura ya tatu ya viwanda tunavyovikusudia ni kuzalisha ajira nyingi. Shabaha yetu ni kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40 ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.
Mheshimiwa Spika;
Nimeamua kulisema hili kwa kirefu sana kwa sababu ili tufanikiwe lazima tuelewane na tusaidiane kulisukuma kwa pamoja jambo hili. 
Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Sekta nyingine ambazo lazima tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza ni kilimo, mifugo na uvuvi. Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani mazao yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi kikubwa ni nchi ya kilimo, ufugaji na uvuvi. Hii inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia 75 wanaishi vijijini na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao na wanazalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula chote kinacholiwa hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25 kwenye pato la taifa yaani GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu ya fedha za kigeni. Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa sekta ya kilimo, mifugo  na uvuvi katika uchumi wetu na maisha yetu ni mkubwa sana. Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika maisha yetu na uchumi wa nchi yetu. Nataka kuahidi kwao sitawaangusha.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu wakulima, wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni watu maskini. Mapato yao yako chini na wanaishi maisha duni. Lengo letu ni kuuimarisha sekta hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi lakini pia ziweze kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadili maisha yao. Tukiweza kuboresha sekta hizi vijana wengi zaidi watavutiwa kujiunga nazo na hivyo kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira. Nataka niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao tutahakikisha zinatekelezwa. Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia kwa dhati ahadi hizo ili kuhakikisha kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa zaidi na wenye tija. Baadhi ya mambo tuliyowaahidi kuyatekeleza ni pamoja na haya yafuatayo:
1.    Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa ikiwa pamoja na ufugaji wa samaki,
2.    Kuwapatia pembejeo,
3.    Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,
4.    Kuwapatia wataalamu wa ugani,
5.    Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,
6.    Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana kufikia lengo hili,
7.    Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa, kule Kagera ina kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda ambako bei iko juu, tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili wakulima wapate bei nzuri. Tutafanya hivyo pia  kwa mazao mengine kama mahindi, chai, pamba, korosho, mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki, n.k.),
8.    Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa wao kuondolewa kwenye ardhi zao kupisha  wawekezaji,
9.    Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya migogoro hiyo tunaviondosha haraka,
10.      Kuhakikisha kwamba tatizo la wavuvi kuvamiwa   na majambazi na uvuvi haramu linashughulikiwa kikamilifu.
Tatizo la Umaskini na Ajira
Mheshimiwa Spika;
Nimezungumzia umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ya matatizo makubwa mawili yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo la UMASIKINI na pili ni tatizo la AJIRA. Ni kweli uchumi wetu umekuwa ukikua kwa kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana na kasi ya kuondoa umasikini na uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana wetu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 28.2 ya Watanzania ni maskini. Na kwamba kwa namna na kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo baina ya matajiri (walionacho) na maskini (wasionacho) linazidi kukua. Tukiendelea hivi tunavyoendelea sasa hatutakuwa tunaitakia mema nchi yetu kwa sababu mgawanyiko mkubwa wa kimapato na tofauti kubwa za kimaisha baina ya matajiri na maskini ukiachiwa uendelee na kuzidi kukua utachochea chuki na uhasama baina ya walionacho na wasionacho. Lazima tujizatiti na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na kuibadilisha hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa watu wetu. Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni uendelezaji wa sekta ya viwanda na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA. Kama nilivyokwisha kugusia, ukuaji wa uchumi wetu haujaenda sambamba na kasi ya watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Tatizo la ajira ni kwa vijana wote waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na ujuzi. Hii inamaana kwamba sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu sizo zinazozalisha ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka msisitizo kwenye sekta ya viwanda hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo ambavyo ndio mwajiri mkubwa hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuweka msisitizo katika Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi kuwawezesha vijana wetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango mbalimbali. Ili hili liwezekane, na sisi tutalifanya, linahitaji mambo mawili makubwa.
Kwanza, kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi. Hatuna budi kuweka mkazo katika viwango vya ubora vya elimu na stadi za kazi wanazopata vijana wetu. Nalisema hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia uendelezaji wa viwanda ikiwa hatujaandaa vijana wenye uwezo, ujuzi, na stadi za kufanya kazi hizo kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu; hatuwezi kutaka kuwekeza katika viwanda vya nguo au samani ikiwa hatuna wahandisi wa mitambo wazuri, wabunifu  wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa na kukubalika. Aidha hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha shughuli za uzalishaji kama hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi na kuiendeleza. Kwa hivyo tutaelekeza nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa shule na vyuo vyetu katika ngazi mbalimbali vinafundisha na kutoa vijana wenye viwango vya hali ya juu vya elimu, maarifa, ujuzi na ufundi.
Mheshimiwa Spika;
Pili, ni suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka kujiajiri. Katika kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua na kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo:
·          Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na fani walizosomea;
·          Kuwawezesha vijana kuanzisha  SACCOS zao na kupitia SACCOS hizo kuwawezesha kupata mikopo;
·          Kuwawezesha vijana wajasiriamali kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na mafao mengine katika mifuko hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Tatu, ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha shughuli za kina Mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda na Maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k. Shughuli za makundi haya zinatusaidia sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa tu na kuzurura zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo wetu wa kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha. Niliahidi, na nataka nirudie hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri zetu, pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na rafiki kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao na shughuli nilizozitaja tutauondoa. Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato, na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali mabilioni ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana mitaani. Viongozi na watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.
Afya
Mheshimiwa Spika;
Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:
·          Kwanza, kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo. Lengo ni kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali ya Rufaa.
·          Pili, tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika Nyanja za afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.
·          Tatu, tutaongeza bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha, tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.
Elimu
Mheshimiwa Spika;
          Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu.  Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.  Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.  Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati.  Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi.
Maji
Mheshimiwa Spika;
          Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi sana ya ukosefu wa maji. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanzisha miradi mipya mikubwa na midogo ya maji kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya uhakika vya maji  ikiwa  pamoja na kuvuna maji ya mvua. Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.
Umeme
Mheshimiwa Spika;
          Suala la upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo katika nchi yetu pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita. Hatuwezi kuzungumzia suala la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi. Serikali yangu itahakikisha kwamba umeme unapatikana wa kutosha na wa uhakika. Tutakamilisha miradi ya umeme iliyopo na kujenga mingine mingi mipya ili wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati ya umeme na viwanda vingi zaidi vidogo vidogo, vya kati na vikubwa vianzishwe.
Madawa ya Kulevya
Mheshimiwa Spika;
          Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike. Familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya taifa imepotea.  Tutaushughulikia mtandao huo hususan wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila ajizi.
Mheshimiwa Spika;
Masuala mengine tutakayoyawekea mkazo katika utawala wa Awamu ya Tano ambayo ninaamini yatasaidia katika kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya Utalii, Mawasiliano, Madini, Ardhi na Makazi, Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara, Ulinzi na Usalama, utunzaji wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Ualbino, Wazee, Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari, wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa masuala haya umefafanuliwa vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Tutayatekeleza ipasavyo.
Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa Spika;
Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.
Mheshimiwa Spika;
Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa na ufisadi. Ndio maana moja ya Imani kuu za CCM ni ile isemayo: “Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa
Kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kuifananisha rushwa na ufisadi ‘Kama Adui Mkubwa wa Watu’.  Akiongea Bungeni Mei 1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
Rushwa [na ufisadi] havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.”
Mheshimiwa Spika;
Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri, wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako tayari kuvumilia upuuzi wa serikali itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.
Mheshimiwa Spika;
Ninafahamu ugumu wa vita niliyoamua kuipigana. Nasema nafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha na rushwa sio watu wadogo wadogo. Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi yetu hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi na utumishi ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu.  Kwa hivyo ili niweze kufanikiwa lazima nipate ushirikiano mkubwa toka kwa Bunge lako tukufu na vyombo vingine vilivyopo na vyenye majukumu ya kupambana na vitendo hivi.
Aidha, tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina mashaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Katika kushugulikia tatizo hili nimeahidi kuunda mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili havitanikwamisha.
Aidha, nataka niahidi mbele ya Bunge lako tukufu kwamba, kiongozi yeyote wa kuteuliwa, ambaye mimi nitakuwa nimemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na ninayo mamlaka ya kumwajibisha, pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya mimi kuchukua hatua hizo hatua na taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Mheshimiwa Spika;
Ninachotaka kusema ni kuwa Serikali yangu itafuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi na watendaji wake ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi. Na tukishajiridhisha hatutasubiri, tutachukua hatua. Ni imani yangu wengine pia katika ngazi mbalimbali mtafanya hivyo. Kwa sababu bila kufanya hivyo rushwa na ufisadi vitazoeleka na kuwa wimbo unaoburudisha badala ya kuudhi na kukera.
Muundo wa Serikali na Utumishi
Mheshimiwa Spika;
Nilipokuwa nazunguka na kuzungumza na wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi, niliahidi kuwa nitaunda serikali ndogo ya wachapa kazi.
Aidha, niliahidi pia kuunda serikali ambayo itawatumikia watu na hasa wananchi wa kawaida. Serikali nitakayounda, nataka iwe inawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu watumishi wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali nitakayoiongoza. Lugha za “hiyo ni changamoto tutaishughulikia”, au “Mchakato unaendeela” hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi Tu. Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza ofisi za umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuwataka watumishi wa Serikali kufanya kazi hatuna budi kuyaangalia na kuboresha mishahara na maslahi yao na mazingira yao ya kufanyia kazi kwa kuwapatia vitendea kazi bora na vya kisasa. Na jambo moja tutakalolitekeleza ni kuangalia namna ya kupunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi yaani PAYE.  Pia tutajitahidi kuwatambua na kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.
Kuongeza Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.  Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi. 
Mheshimiwa Spika;
Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo tutayasimamia kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza, safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.
Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
·          Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;
·          Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;
·          Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;
Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.
          Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za walimu ngapi?, madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.
Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.
Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha ambayo kwa kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya Serikali.
Nne, tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba. Ni matarajio yangu kutakapoleta Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono.
Tano, tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu ununuzi wa bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Samani zote kwa ajili ya matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa hapa hapa nchini.
Sita, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu na kuthibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi waandamizi wa Serikali; na
Saba, tutaendelea kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na Taasisi zake zote yasiyo na tija kwa uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika;
          Kwa ajili hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia kuiunda vitakuwa ni: kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali; kubana matumizi kwa kupunguza yale ambayo kutokana na hali yetu ya uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika; na kurejesha nidhamu ya  Serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.
          Tutatekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja na mambo mengine kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri; kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha kwamba wale wote wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu ya matumizi ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na waajiri wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kubainisha maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaigharimu Serikali fedha nyingi na kuyadhibiti. Aidha, nitoe wito kwa Watanzania wote kila mmoja wetu afanye kazi iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni, n.k.  Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka kwa Watanzania kutokupenda kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi vijiweni, muda ambao ungetumika kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu yangu ni HAPA KAZI TU!
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kikanda na Kimataifa
Mheshimiwa Spika;
          Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja ya diplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika awamu zilizotangulia za uongozi. Serikali yangu itaendeleza sifa hiyo kwa kujenga juu ya msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa waumini na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu. Tutaendelea kuwa waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na daima tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi wanachama. Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano wetu hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama ambao tunauhusiano wa kihistoria na kidugu. Tutaendelea kuamini katika Umoja wa Afrika (AU) na azma ya ndoto ya waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika. Tutaendelea pia kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na kushirikiana na nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu ya amani, usalama na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.
          Tutaendeleza na kustawisha mahusiano na marafiki zetu wote Magharibi, Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi zetu na watu wetu. Tutapenda kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri kisiasa kukuza mahusiano yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi. Tutafanya hivyo pia kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu na Umoja wa Mataifa (UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), n.k.
Aidha, tutazitaka Balozi zetu zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya fedha tunazowapelekea hususan katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na mchango wao katika ukuzaji wa sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia yetu na Sera yetu ya nje ikijibu changamoto zetu za ndani za ajira, miundombinu, masoko ya mazao ya wakulima, viwanda n.k.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika;
Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Bunge hili linalo nafasi ya kuweka historia ya kuwa kitu kimoja na kuweka masilahi ya Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha za vijembe, mipasho, na ushabiki wa vyama bungeni. Kwanza, tukumbuke wote bila kujali itikadi za vyama vyetu sisi ni kitu kimoja; na pili tumechaguliwa kuwawakilisha wenzetu. Baada ya miaka mitano kila mmoja atarudi kwenye jimbo lake kuomba kura na huko atapimwa kwa maendeleo aliyopeleka. 
Tusimame pamoja, Tanzania ni yetu sote tutangulize masilahi ya nchi mbele, na kwa mara ya kwanza Watanzania waone Bunge tofauti na sio Bunge la kuzomea, kutoka nje, kutukanana, mipasho, n.k. Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge hili Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.
Aidha, napenda kusisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa. Matarajio na matumaini ya Watanzania waliotuchagua na kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni makubwa. Wanachotaka kuona ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na mimi, baada ya miaka mitano toka sasa, tutapimwa kwa namna tutakavyokuwa tumetekeleza mambo ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu. Mimi nina amini kabisa kwa ushirikiano wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu tutaweza kuzitimiza ndoto za Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Spika;
Sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!
Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!

Ahsanteni kwa kunisikiliza.