Mwaka 2001, mwezi Desemba katika milima ya Tora Bora baada
ya mapambano ya siku kumi na moja toka tarehe 6 hadi 17 na mabomu kadhaa
kudondoshwa katika milima hiyo hatimaye askari wa miguu walianza zoezi
la kuikagua milima hiyo kuangalia kama kuna masalia yoyote muhimu
yanayoweza kuwapa fununu ya kuielewa vita waliyoianzisha kati yao
Majeshi ya Marekani na Wanamgambo wa Taliban.
Katika mchakato huo wa ukaguzi wanajeshi wa marekani
walifanikiwa kumuokota kijana mmoja wa umri wa mika 21 akiwa hai. Baada
ya kumuokota wanajeshi kadhaa wakampakia katika chopa ya kivita na
kurudi nae katika kambi ya kijeshi ya Bagram Air Base iliyo nchini
Afghanistan.
Baada ya kufika katika kambi ya Bagram wanajeshi wakaanza
kumuhoji kijana huyo ajieleze yeye ni nani na alikuwa anafanya nini
katika milima ya Tora Bora.
Baada ya kujitambulisha kijana huyo akawaeleza kuwa alikuwa
anawinda katika milima hiyo ya Tora Bora na kwa bahati mbaya akajikuta
ameingia kwenye eneo ambalo hakujua kuwa kulikuwa na mapigano ya
kijeshi.
Maafisa wote wa kijeshi hawakuamini maelezo haya na
waliendelea kumuhoji kwa siku kadhaa lakini yule kijana alishikilia
maelezo yake yale yale kuwa alikuwa anawinda milimani.
Baada ya kutokuwepo kwa mafanikio yoyote ya kumuhoji kijana
huyu Maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi katika kituo cha Bagram
wakawasiliana na maafisa wa CIA waliopo nchini Afghanistan na kuwaeleza
juu ya tukio hilo. Maafisa hao wakawashauri kuwa kijana huyo wakabidhiwe
wao ili wamuhoji wao kwa kina.
Siku tatu baadae kijana huyo akakabidhiwa kwa maafisa wa
CIA na wao wiki moja baadae wakamsafirisha kutoka Afghanistan mpaka
kwenye jela za siri (Black Sites) za CIA zilizopo ulaya katika nchi ya
Romania na baadae akaamishiwa jela za siri nchini Poland.
Baada ya kijana huyo kufikishwa huko mahojiano yakaendelea
na akaendelea kushikilia msimamo wake kuwa alikuwa anawinda kwenye
milima ya Tora Bora. CIA ikaamua kupanua wigo wake zaidi ili wamtambue.
Wakachukua alama zake za vidole na kuziingiza katika mfumo wa alama za
vidole wa nchi karibia zote za kiarabu lakini wakapata matokeo sifuri,
hakukuwa na taarifa zozote zinazoshabihiana alama za vidole za kijana
huyo.
Hii ilikuwa na maana nyingi lakini maana moja kubwa ni
kwamba kijana huyu hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu katika maisha
yake, alikuwa ni 'raia mwema'!
CIA wakaanza kuhisi labda kijana huyu kweli hakuwa na hatia
yoyote. Lakini kabla hawajalipa nafasi wazo hilo kukua kwenye vichwa
vyao, wakaakua wafanye kitu cha kubahatisha, wakaingiza alama za vidole
za kijana huyo katika mfumo wa kiusalama wa nchini kwao marekani na
matokea ambayo waliyapata hakuna ambaye aliweza kuamini.
Kumbukumbu za mifumo ya kiusalama ya nchi za marekani
zilionyesha kuwa mtu mwenye alama hizo za vidole zinafanana kabisa na
mtu ambaye alijaribu kuingia nchini marekani siku ya tarehe 3 Agosti
2001 katika uwanja wa ndege wa Orlando, Florida akitokea Dubai.
Maafisa wa uhamiaji wa uwanja wa ndege wakamkataa kuingia
nchini marekani kutokana na sababu kadhaa. Kwanza kijana huyo alikuwa na
fedha dola 2,800 pekee na hii iliwapa shida maafisa wa uhamiaji kuelewa
angewezaje kuishi nchini marekani? Pili kijana huyu alikuwa amekata
tiketi ta kwenda pekee (one way ticket).
Sababu hizi mbili zilipelekea maafisa wa uhamiaji wa uwanja
wa ndege kuhisi kijana huyu alikuwa na mpango wa kuwa muhamiaji haramu
kwani dalili hizo zilionesha kuwa hakuwa na mpango wa kurudi tena kwao.
Hivyo basi maafisa hao wa uhamiaji wa uwanja wa ndege wa Orlando
wakamkataa kijana huyo juingia nchini marekani na wakamrudisha
alikotokea.
Maafisa wa CIA walishitushwa na jambo hili na wakawasiliana
na vyombo vingine vya usalama nchini Marekani na pasipo kupoteza muda
maafisa kutoka shirika la upelelezi la FBI wakafika katika uwanja wa
ndege wa Orlando, Florida ili wapate taarifa zaidi kuhusu nini hasa
kilitokea siku ya Agosti 3 2001 siku ambayo kijana huyo alikataliwa
kuingia nchini marekani.
Baada ya FBI kufika uwanja wa ndege waliomba kuzungumza na
maafisa uhamiaji waliokuwepo siku ya tarehe 3 Agosti pia waliomba
wapatiwe mikanda ya video ya kamera za ulinzi za uwanja wa ndege.
Baada ya kuangalia mikanda hiyo ya video, FBI waligundua
jambo kubwa zaidi ambalo hawakulitegemea kabisa. Kamera za ulinzi zilizo
nje ya uwanja zilirekodi gari inayomilikiwa na Mohamed Atta likiwa
limepaki nje ya uwanja wa ndege.
Kwa wasiomfahamu Mohammed Atta ndiye alikuwa mtekaji
kiongozi wa watu walioteka ndege za kimarekani na kwenda kuzigongesha
katika magorofa ya WTC siku ya tarehe 11, Septemba 2001. Pia ndiye
aliyeendesha moja wapo ya ndege hizo zilizotekwa.
Kwahiyo FBI wakang'amua kuwa siku hiyo Mohammed Atta
alifika uwanja wa ndege kumpokea kijana huyo lakini kwa bahati mbaya
maafisa uhamiaji walimkataa asiingie Marekani.
Hii ilikuwa na maana kwamba kama kijana huyu asingelitiliwa
shaka na maafisa wa uhamiaji basi alitakiwa kuwa mojawapo ya washiriki
walioteka ndege na kuzilipua katika majengo ya WTC siku ya Septemba 11,
2001.
Taarifa hizi ziliishitua FBI na pasipo kuchelewa
wakawataarifu maafisa wa CIA katika jela ya siri nchini Poland ambako
kijana huyu alikuwa anashikiliwa, na baada ya maafisa hawa kupata
taarifa hii mara moja wakawasiliana na Makao Makuu ya CIA Langley,
Virginia nchini Marekani.
Mara baada ya taarifa hizi kufika Makao Makuu ya CIA,
Mkurugenzi wa CIA Bw. Leon Panetta akaamuru kijana huyo awekwe 'mahali
salama' kwa ajili ya 'mahojiano' zaidi.
Ndege ikaandaliwa na safari ya kuelekea gereza la Guantanamo Bay ikaanza.
Jina halisi la kijana huyu anaitwa Mohammed al-Qahtani
kipindi anakatwa alikuwa na umri wa miaka 21 na kwa sasa ana miaka 36 na
ni mfungwa namba 63 (ISN 10063) katika gereza la Guantanamo Bay.
NDANI YA GUANTANAMO: 'MAHOJIANO' ZAIDI
Baada ya kijana al-qahtani kufikishwa katika gereza
Guantanamo ambapo aliwekwa selo katika jengo lililoitwa Camp Delta
'mahojiano' zaidi yakaendelea. Licha ya mambo yote ambayo vyombo vya
usalama viligundua juu yake lakini kijana yule aliendelea Kushikilia
msimamo wake kuwa alikuwa anawinda kwenye milima ya Tora Bora.
Ilifikia hatua mpaka Katibu mkuu kiongozi wa makamu wa rais
wa kipindi hicho Bw. David Addington pamoja na mshauri wa ikulu Bw.
Alberto Gonzales walifika binafsi katika jengo la Camp Delta ndani ya
gereza la Guantanamo mahsusi kwaajili ya kuongea na kijana al-qatani ili
aeleze ukweli lakini kijana huyo akashikilia msimamo kuwa yeye ni
muwindaji.
Ndipo hapa ilipofikia hatua hii Waziri wa Ulinzi wa
Marekani wa wakati huo akaidhinisha 'Mbinu za Mahojiano Zilizoboreshwa'
(Enhanced Interrogation Techniques) zitumike kumuhoji kijana huyo.
Mbinu hizi zilizoboreshwa zilikuwa zinajumuisha kwa mfano
kutesa mfungwa kwa kumnyima pumzi kimateso kwa kumiminia maji
(waterboarding), mikao ya msongo (stress positions), kumnyima usingizi
n.k.
Uamuzi huu ulikuja kuleta mushkeli na watu wa haki za binadamu miaka iliyofuata.
Baada ya maafisa waliokuwa wanamuhoji kupewa idhini ya
kutumia 'mbinu zilizoboreshwa' inasemekana kwamba kijana al-Qahtani
ndiye mmoja wa wafungwa wa Guantanamo waliovunja rekodi kwa kuhojiwa
muda mrefu zaidi kwa 'mbinu zilizo boreshwa'. Inasemekana kijana
al-Qahtani alihojiwa kwa siku 48 mfululizo!
Baada ya 'mahojiano ya kina' yaliyochukua siku 48 kwa
kutumia 'mbinu zilizoboreshwa' hatimae al-Qahtani akafunguka na kueleza
ukweli.
Kwanza akakiri kuwa jina lake ni Mohammed al-Qahtani na ni raia wa Saudi Arabia.
Kwanza akakiri kuwa jina lake ni Mohammed al-Qahtani na ni raia wa Saudi Arabia.
Pia akakiri kuwa ni yeye ndiye aliyekataliwa kuingia nchini
Marekani siku ya Tarehe 3, Agosti 2001 na akaeleza kuwa alipewa maagizo
na mtu anayeitwa Khalid Sheikh Mohammed ili aje marekani kwaajili ya
kazi maalumu. Pia alieleza kuwa aliwahi kupatiwa mafunzo maalumu ya
utendaji wa kishushushu na mawasiliano ya usiri (Operational training in
Covert Communications) na aliyempatia mafunzo hayo alijulikana kama Abu
Ahmed al-Kuwait.
Baada ya kupewa maelezo haya ilikuwa ni hatua kubwa kiasi kwa CIA lakini bado kulikuwa na mambo kadhaa hayakuwa sawia.
Kwa upande Khalid Sheikh Mohammed (KSM) mtu ambaye kijana
huyu alimtaja kuwa ndiye alyemuagiza aje Marekani, mtu huyu alikuwa
anafahamika vizuri na CIA. Walimfahamu kuwa ndiye moja wa Lutenati wa
ngazi za juu wa kikundi cha Al Qaeda na ndiye 'mchora ramani' wa
mashambulizi ya septemba 11, 2001.
Lakini mtu wa pili (Abu Ahmed al-Kuwait) aliyetajwa na huyu
kijana kuwa ndiye aliyempatia mafunzo kijana juu ya ushushushu na
mawasiliano ya siri, mtu huyu CIA walikuwa hawamfahamu. Ndio ilikuwa
mara yao ya kwanza kulisikia jina hilo.
Hivyo basi kipaumbele kikawekwa kwamba kijana huyu
'ahojiwe' zaidi ili atoe taarifa zitakazofanikisha kumpata KSM (Khalid
Sheikh Mohammed) 'mchora ramani' wa mashambulizi ya Septemba 11.
Mahojiano kwa kutumia mbinu zilizobordshwa yakaendelea.
Kwa msaada wa maelezo waliyoyapata kutoka kwa kijana
al-Qahtani maafisa wa CIA kwa kushirikiana na maafisa wa ISI
(Inter-Service Intelligence - Idara kuu ya masuala ya usalama na
ushushushu nchini Pakistani) walifanya oparesheni maalumu ya kumkamata
KSM (Khalid Sheikh Mohammed) baada ya kumuwinda kwa muda mrefu sana na
hatimae siku ya Machi 1, 2003 walifanikiwa kumkamata KSM akiwa hai
katika katika jimbo la Ralwapindi nchini Pakistani.
Baada ya kukamatwa tu na taarifa hiyo kufika makao makuu ya
CIA Langley, Mkurugenzi mkuu Bw. Panetta akaamuru KSM awekwe 'mahali
salama' mara moja. Na pasipo kupoteza muda siku hiyo hiyo CIA
wakampandisha ndege KSM na kumpeleka gereza la Guantanamo. Na baada ya
KSM kupokelewa Guantanamo alipewa selo kwenye jengo mojawapo la
Guantanamo linaloitwa Camp Echo na akatambulika kama mfungwa namba ISN
10024.
Kesho yake 'mahojiano ya kina' yakaanza kwa kutumia 'mbinu zilizoboreshwa'.
Haikuchukua siku nyingi za 'mahojiano' KSM akaanza
kufunguka na kusema ukweli. Kwanza akakiri kuwa yeye ndiye 'mchora
ramani' wa shambulizi la Septemba 11, na ni moja ya malutenati
wanaotegemewa na Al Qaeda katika kueneza propaganda za kikundi hicho.
Akakiri kuhusika kutafuta vijana watakaotekeleza shambulizi hilo,
akakiri kusaidia baadhi yao kupata mafunzo ya urubani na akakiri
kusaidia kuwaingiza marekani vijana hao.
Maafisa wa jeshi na CIA walimbana zaidi KSM aeleze ni namna
gani wanaweza kuwapata viongozi wa ngazi za juu wa Al-Qaeda na hasa
hasa kiongozi mkuu lakini jibu la KSM liliwashangaza kila mtu. KSM
akawaeleza kuwa hata yeye afahamu kiongozi mkuu yuko wapi au
anapatikanaje.
Mwanzoni walihisi anawadanganya lakini baada ya 'kumbana'
zaidi wakagundua kuwa anamaanisha kuwa hajui 'kiongozi mkuu' yuko wapi
wala namna ya kumpata.
KSM akawaeleza kuwa kiongozi mkuu, Osama Bin Laden aliacha
kutumia simu toka mwaka 1998 maada ya mawasiliano yake ya simu ya
satelaiti kudukuliwa na CIA na kuponea chupu chupu kuuwawa na wanajeshi
wa kimarekani.
Akawaeleza kuwa tangu hapo aliacha kutumia na mawasiliano
ya simu na mawasiliano yote mengine ya kisasa na kwa upande wa
mawasiliano akawa muumini wa falsafa ambayo imekuja kutumiwa na karibia
maafisa wote wa ngazi za juu wa vikundi vya wapiganaji katika mashariki
ya kati, kwamba; "If you live like you are in the 'past', the 'future'
will never find you"! (Ukiishi kama upo kwenye nyakati za zamani, usasa
hautakukamata kamwe).
Kwa hiyo mawasiliano yote yalikuwa yanafanyika kwa mdomo kutoka kwa mtu kwenda kwa mtu au kwa barua za kuandika kwa mkono.
CIA wakambana zaidi aeleze je yeye alikuwa anapataje
maagizo kutoka kwa kiongozi mkuu na akawajibu kulikuwa na mtu mmoja tu
ambaye alikuwa anaaminika kwa asilimia mia moja na kingozi mkuu na ndiye
aliyekuwa 'mpambe' wa karibu wa Bin Laden na kwamba kwa miaka kadhaa
wapiganaji wa Al-Qaeda wala malutenati wa ngazi za juu walikuwa
hawajawahi kumuona Bin Laden wala hawajui alipo na maagizo yote
waliyapata kwa mdomo kutoka kwa mtu mmoja pekee aliyeitwa Abu Ahmed
al-Kuwait.
Maafisa wote wa jeshi na CIA waliduwaa. Hii ilikuwa ni mara
ya pili wanasikia jina hili. Mara ya kwanza walilisikia kutoka kwa
kijana al-Qahtani kuwa alipatiwa mafunzo ya ushushushu na Abuu Ahmed
al-Qahtani na sasa wanaelezwa na KSM ambaye ni lutenati wa ngazi za juu
kabisa wa Al Qaeda kuwa hajawahi kumuona kiongozi mkuu kwa miaka kadhaa
na maagizo yote yalikuwa yanaletwa kwake na mtu anayeitwa Abu Ahmed
al-Kuwait.
Kitu kilichowasahangza zaidi CIA ni kwamba walikuwa
wanawafahamu viongozi na malutenati wote wa ngazi za juu wa Al Qaeda
lakini jina hili lilikuwa jipya kwao. Hawakuwahi kumsikia Abu Ahmed
al-Kuwait.
Wakiwa bado wapo kwenye mshangao wapigani wa kikurdi kutoka
nchini Iraq wakawasiliana na serikali ya marekani kuwaeleza kuwa
wamemkamata Hasaan Ghul moja ya mawakala wa Al Qaeda anayetegemewa
nchini Iraq.
CIA wakampakia Hassan Ghul kwenye ndege na kumpeleka kwenye jela za siri nchini Romania.
CIA wakampakia Hassan Ghul kwenye ndege na kumpeleka kwenye jela za siri nchini Romania.
Baada ya 'kumuhoji' kwa siku kadhaa Hassan Ghul akawaeleza
kuwa maagizo yote kuhusu mashambulizi na mipango mingine anayapata
kutoka kwa kiongozi mkuu Osama Bin Laden kupitia kwa mtu anayemfahamu
kwa jina la Abu Ahmed al-Kuwait.
Mshangao wa CIA ukageuka kuwa kitendawili. Huyu Abu Ahmed al-Kuwait ni nani na wanawezaje kumpata?
Mkurugenzi Mkuu wa CIA akaamuru kuwa kumtambua na kumkamata Abu Ahmed al-Kuwait kiwe kipaumbele namba moja..
Baada ya mchakato wa muda mrefu hatimae mwaka 2007 CIA
walifanikiwa kumtambua Abu Ahmed al-Kuwait ni nani! Wakafanikiwa kupata
jina lake halisi (Ibrahim Saeed Ahmed) na kwamba mwanzoni alikuwa ni
mwanafunzi wa KSM kabla hajapanda ngazi kuwa mpambe wa Bin Laden.
Baada ya kumfahamu kwa kiasi CIA wakaanzisha mpango maalum
wa kumchunguza ili wapate taarifa zaidi juu yake. Ili waweze kumpata
kirahisi CIA wakafanya zoezi maalum la kuwatambua ndugu zake mbali mbali
waliokuwa wanaishi kwenye nchi tofauti tofauti za kiarabu.
Baada ya kuwatambua ndugu hao CIA wakafanya kazi ya kudukua
mawasiliano ya simu ya ndugu zake na katika kitu kimojawapo ambacho
walikigundua ni kwamba ndugu zake hao walikuwa na desturi ya kuwasiliana
na namba za simu tofauti tofauti lakini zote zikiwa ni za Pakistan. Hii
ilipelekea CIA kuhisi kwamba namba hizi ni za al-Kuwait lakini alikuwa
anazibadilisha mara kwa mara ili kuepuka kugundulika.
Kwahiyo walichofanya CIA ni kusubiri siku ambayo ndugu
yoyote wa al-Kuwait akipiga simu yoyote kwenda nchi ya Pakistan basi
wataifuatilia namba hiyo ili wafahamu ni nani aliyekuwa anaongea naye.
Siku hiyo haikukawia sana kwani mwaka 2010 ndugu mmoja wapo
alipiga simu kwenda Pakistan katika mji wa Pashwar. Kwa kutumia
Wapalestina waliokuwa wanafanya kazi kwaajili ya CIA waliifuatilia simu
hiyo mjini Pashwar na kuthibitisha kuwa aliyekuwa anaongea na simu hiyo
alikuwa ni Abu Ahmed al-Kuwait. Baada ya al-Kuwait kumaliza kuongea na
simu aliingia ndani ya gari na kuondoka na wapelelezi hao wakamfutilia
kwa makini wajue anakoelea.
Pasipo kujua kuwa anafuatiliwa al-Kuwait aliendeshe gari
mpaka mji wa Abbottabad. Na alipofika Abbottabad akaingia kwenye Jumba
moja la kifahari. Jumba hili lilikuwa na muonekano na ulinzi uliotia
shaka. Na hii ikapelekea CIA kuamini kuwa ndani ya jumba hilo hakuwa
al-Kuwait pekee anayeishi bali kuna uwezekano mtu wa hadhi ya juu zaidi
alikuwa anaishi humo ndani. Pengine labda kiongozi mkuu wa Al Qaeda,
Osama bin Laden labda alikuwa ni mkazi humo ndani.
Waziristan Haveli
Baada ya CIA kugundua nyumba hii na kuitilia mashaka kuwa
kuna uwezekano inamuhifadhi kiongozi wa hadhi ya juu wa Al Qaeda pengine
labda Osama bin laden mwenyewe, hivyo wakaingiza wapelelezi katika mji
wa Abbottabad ambao walinunua nyumba mjini hapo kama raia mwingine wa
kawaida. Baada ya wapelelezi hao kufanikiwa kufanya mkazi mjini
Abbottabad wakaanza kazi ya kukusanya taarifa juu ya jumba hilo na
wakazi wake.
Wapelelezi hao ambao walikuwa ni raia wa Pakistan
wanaofanya kazi kwa niaba ya CIA wakaanza kuwadodosa majirani na
wakafanikiwa kupata taarifa za kutosha kiasi.
Kwanza majirani waliwaeleza kuwa jumba hilo linamilikiwa na
mtu wanayemfahamu kama Arshad Khan (Abu Ahmed al-Kuwait) ambaye anaishi
na kaka yake pamoja na familia zao. Majirani wakaeleza kuwa Arshad
amewaeleza kuwa kuwa yeye ni msimamizi wa biashara za Hoteli za familia
yao zilizopo Dubai. Pia majirani walimueleza kuwa Arshad (al-Kuwait)
alikuwa ni 'mtu wa watu' na alikuwa anahudhuria karibia kila msiba
mtaani kwao.
Pia walielezwa kuwa licha ya kuwa na uwezo wa kifedha huwa
anapenda kufanya manunuzi ya mahitaji yake ya nyumbani hapo hapo mtaani
na mara kwa mara hutoka na watoto wake kwenda kuwanunulia mikate kwenye
duka la uokaji (bakery) mtaani hapo.
Pia majirani waliwaeleza kuwa wamezoea kuliita jumba hilo
Waziristan Haveli (Waziristan Mansion (Kasri la Waziristan)) kwani
waliamini kuwa wakazi wa jumba hilo wanatokea Waziristan.
Baada ya CIA kupata taarifa hizi kutoka kwa wapelelezi
waliojipenyeza mtaani hapo wakaamua wapanue wigo zaidi kwa kuwahusisha
kitengo Maalumu cha Taifa la Marekani chini ya wizara ya ulinzi (DOD)
kinachohusika na kukusanya taarifa na Ushushushu wa kijiografia
(National Geospatial-Inttelligence Agency - NGA) ili wafahamu nukta
baada ya nukta ya jumba hilo.
Kwa kutumia picha za satelaiti na kukusanya picha kwa
kutumia ndege inayojiendesha yenyewe (drone) NGA walipata taarifa zote
muhimu kuhusu jumba hilo kuziwasilisha CIA.
Taarifa yao ilieleza kuwa jumba hilo lililoitwa Waziristan
Haveli lipo umbali wa takribani kilomita moja na nusu kutoka kituo cha
mafunzo ya kijeshi cha Abbottabad cha jeshi la Pakistan. Mtaani ambao
jumba hili lilikuwepo ulikuwa na makazi ya wastaafu wengi wa jeshi la
Pakistan.
Jumba hili lilichukua eneo kubwa zaidi kuliko nyumba
nyingene za jirani kwani jumba lilijengwa kwenye eneo la ardhi lenye
ukubwa la takribani mita za mraba 3,500.
Jumba hili lilizungukwa na ukuta wenye urefu wa futi 12
lakini ndani yake ukiingia unakutana na eneo la wazi tupu alafu anakuta
ukuta mwingine wenye urefu wa futi 18. Kuta zoto hizi juu yake zilikuwa
na waya za miba miba na umeme.
Pia jumba hili lilikuwa na ghorofa tatu na katika balkoni
ya gorofa ya tatu ilikuwa na ukuta wake wa kuikinga wenye urefu wa futi
7. Pia kulikuwa na kamera za ulinzi katika kila kona ya jumba hili.
Pamoja na hayo pia NGA waligundua kuwa ndani ya jumba hilo
kulikuwa na bustani kubwa iliyopandwa mboga mboga, pia kulikuwa na kuku
zaidi ya 100, sungura pamoja na ng'ombe mmoja.
Pia jumba hili lilikuwa na mdirisha madogo na machache
kiasi kwamba ukiliangalia haraka haraka unaweza kudhani halina madirisha
kabisa.
Pia idara ya ushushushu wa kijiografia ya Marekani NGA
ilifanikiwa kukusanya taarifa za wakazi wa jumba hilo ambapo
walifanikiwa kung'amua kuwa Kasri hilo lilikuwa na wakazi wapata 22
wanaoishi ndani yake wengi wao wakiwa ni watoto. Pa waling'amua kuwa
kulikuwa na takribani wakazi watani ambao kamwe walikuwa hawatoki nje ya
jumba hilo.
Baada ya NGA kuwasilisha taarifa yao kwa CIA kuhusu vile
walivyovibaini kuhusu jumba hili, Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Leon
Panetta alizidi kushawishika kuwa Kasri hili lilikuwa linamuhifadhi
kiongozi wa hadhi ya juu wa Al Qaeda na pengine ni Bin Laden mwenyewe
anaishi humo.
Hivyo basi akaamuru ufanyike uthibitisho wa mwisho kuhakiki kama ni kweli kile anachokihisi.
Hivyo basi akaamuru ufanyike uthibitisho wa mwisho kuhakiki kama ni kweli kile anachokihisi.
CHANJO FEKI
Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena alitaka kwanza kuhakiki
kama hisia zao ni za kweli kuwa Bin Laden anaishi kwenye Kasri hilo.
Hivyo basi maafisa wa CIA wakaja na mpango kuwa wafanye uhakiki wa uwepo
wa familia yake na kama familia yake ipo kwenye jumba hilo basi hapana
shaka Bin Laden atakuwepo ndani ya hilo Kasri.
Kwahiyo maafisa hao wakaemweleza mkurugenzi wao
wanachotakiwa ni kupata sampuli za vinasaba (DNA) za watoto wanaoishi
ndani ya jumba hilo.
Kwahiyo mkakati ukawekwa kwamba ifanyike chanjo feki ili wapate fursa ya kuingia kwenye jumba hilo kuwahudumia watoto na wakifanikiwa kuingia watatumia mbinu kadhaa kuchukua sampuli za vinasaba za watoto eidha kwa kubakiza damu kiduchu za hao watoto kwenye sindano ya kutolea chanjo au mbinu nyinginezo.
Kwahiyo mkakati ukawekwa kwamba ifanyike chanjo feki ili wapate fursa ya kuingia kwenye jumba hilo kuwahudumia watoto na wakifanikiwa kuingia watatumia mbinu kadhaa kuchukua sampuli za vinasaba za watoto eidha kwa kubakiza damu kiduchu za hao watoto kwenye sindano ya kutolea chanjo au mbinu nyinginezo.
Ili kufanikisha azma hii CIA walimuendea Daktari Bingwa
aliyeitwa Shakil Alfridi ambaye alikuwa ndiye daktari mkuu katika maeneo
ya Khyber mpakani na Afghanistan.
CIA wakafanikiwa kumshawishi daktari Hugo ashiriki kwenye mpango huo wa kutoa chanjo hiyo feki.
Baada ya kufanikiwa kumshawishi Dk. Shakil matangazo
yakawekwa kuhusu mpango wa kutoa chanjo katika eneo hilo kwa mwezi
February na Mwezi April 2011. Ili kuwapiga chenga serikali ya mji wa
Abbattobbad wasihusike kwenye zoezi hilo Dk. Shakil alieleza kuwa
amepata ruzuku kutoka mashirika ya kimataifa ili atoe chanjo hiyo bure
na chanjo hiyo ni ya kuwakinga watoto dhidi ya Hepatitis B.
Hivyo basi alifanya zoezi lake kwa Uhuru pasipo kuingiliwa
na watu wa serekali za mitaa na manesi ambao walijumuika nae kutoa
chanjo hiyo walipata posho iliyoshiba.
Ili kuepuka watu kuanza kuuliza maswali na kuwa na
wasiwasi, alianza kutoa chanjo hiyo katika mitaa wanayoishi masikini
kama vile mitaa ya Nawa Sher. Alifanya hivyo kwa mwezi February na
aliporejea tena alitoa chanjo hiyo katika mtaa wanaoishi watu matajiri
katika mji wa Abbattobad yaani mtaa wa Tabil ambapo ndipo kulikuwa na
hilo jumba linalotiliwa mashaka.
Ilipofika zamu ya kutoa chanjo kwa watoto waliopo ndani ya
hilo jumba walikaribishwa kwa ukarimu na Dk. Shakil mwenyewe akabaki nje
getini na akamruhusu nesi aliyeitwa Bakhto aingie ndani ya kasri atoe
'chanjo' kwa watoto.
'Chanjo' ikatolewa, zoezi likaisha Dk. Shakil na manesi wake wakarejea Khyber na kukabidhi sampuli walizozipata kwa CIA.
Sampuli zikasafirishwa mpaka marekani, zikafanyiwa
uchambuzi wa DNA kisha ikalinganishwa na DNA ya dada yake Osama Bin
Laden aliyefariki dunia mwaka 2010 jijini Boston nchini Marekani kwa
uvimbe kichwani.
Baada ya sampuli hizo za DNA kupimwa na kulinganishwa,
majibu yakapelekwa mezani kwa Mkurugenzi Mkuu wa CIA Bw. Pattena. Baada
ya Pattena kuyaona majibu hayo akatabasamu mpaka ufizi wa mwisho,
akainua simu ya mezani na kupiga ikulu ya Marekani na kuomba kuongea na
Rais Obama.
Mara baada ya kuunganishwa na Rais Obama, Pattena akampa
taarifa Rais, taarifa iliyosubiriwa muda mrefu na kwa shauku kubwa, kwa
kifupi akamueleza Rais kwa furaha "we got him.!" ("Tumempata.!")
OPARESHENI NEPTUNE SPEAR
Baada ya kupatikana uhakika kuwa Osama Bin Laden anaishi
ndani jumba hilo lililopo Abbottabad, CIA wakafanya kikao maalum na
Jemedali Msaidizi (Vice Admiral) William H. McRaven ambaye ni kamanda wa
kitengo maalum kinachosimamia oparesheni maalum zinazofanywa na majeshi
yote ya marekani ( Joint Special Operations Command - JSOC) ambapo
katika kikao hicho CIA walimpa taarifa wa kila wanachokifahamu kuhusu
makazi hayo waliyoyagundua.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, Admiral McRaven akapendekeza
kuwa wanaweza wakatuma kikosi cha makomando kufanya uvamizi kwenye jumba
hilo lakini akawa na wasiwasi inaweza kuleta mushkeli na jeshi la
Pakistan ambalo lipo kilomita moja na nusu tu kutoka makazi ya siri ya
Bin Laden.
Baada ya majadiliano ya kina Admiral McRaven akawaagiza
maafisa kadhaa kutoka Jeshi la Wanamaji (U.S. NAVY) kitengo cha
Maandalizi ya ya Mapigano/vita Maalum ( Special Warfare Development
Group - DEVGRU) kwamba waweke ofisi ya muda makao makuu ya CIA Langley
na washirikiano kuandaa mpango maalumu utaoenda kupendekezwa kwa Rais
juu ya kushugjulikia makazi yaliyoaminika kumficha Osama Bin Laden.
Baada ya miezi miwili ambayo DEVGRU waliitumia kuaandaa
mpango kwa kushirikiana na CIA hatimaye wakawasilisha mapendekezo yao
kwa Mkurugenzi wa CIA Bw. Pattena na kwa waziri wa ulinzi Bw. Robert
Gates.
Kisha Rais Obama akaitisha kikao maalum cha Baraza/kamati ya usalama ya Taifa ili kujadili suala hilo.
Baada ya majadiliano marefu kwenye kikao hicho ilionekana
kuwa Rais Obama alipendelea zaidi pendekezo la kulipua makazi hayo kwa
bomu kutoka angani. Lakini maswali yakaibuka je ni vipi kama kuna
handaki kwenye jumba hilo na Osama labda huwa anakaa chini ya hilo
handaki. Katika upelelezi wao wote CIA hawakuweza kung'amua kama
kulikuwa na handaki katika jumba hilo ama la.
Kwa kuzingatia hivyo basi (uwepo wa handaki) kama wataamua
kulipua makazi hayo kwa bomu basi itawabidi watumie bomu lenye uzito
usiopungua Kg. 910 ili liweze kusambaratisha kabisa makazi hayo pamoja
na handaki kama lipo.
Lakini pendekezo hili nalo likawa na changamoto zake kwani
kama litatumika bomu lenye nguvu kubwa hivyo, kulikuwa na nyumba kadhaa
za majirani ambazo zitakuwa ndani ya kipenyo cha mlipuko (blast radius).
Pia kama makazi hayo yangelipuliwa kwa bomu kusingekuwa na ushahidi
wowote wa kujiridhisha kuwa Osama ameuawa kwenye shambulio hilo.
Baada ya kubainishwa kwa changamoto hizi katika kikao
kilichofuata cha kamati ya Usalama wa Taifa, Obama akasitisha mpango huo
wa kulipua makazi kwa bomu usitekelezwe.
Chaguo la pili lilikuwa kwa makomando wa kikosi cha
Wanamaji (Navy) SEALs, wavamie makazi hayo kwa kutumia helikopta maalum
zinazoruka bila kutoa kelele na sio rahisi kuonekana na Rada ya adui.
Chaguo hili lilikuwa ni zuri lakini lilikuwa na changamoto moja kubwa.
Kumbuka makazi haya yapo karibu kabisa na kituo cha Kijeshi cha
Pakistani, itakuwaje kama wakishtukiwa kabla hawajamaliza kutekeleza
oparesheni?
Baadhi ya watu waliokuwepo kwenye kikao akiwemo waziri wa
ulinzi Bwa. Robert Gates akapendekeza kuwa labda wawashirikishe watu wa
kitengo maalumu cha ushushushu cha Pakistan (ISI). Wazo hili likapingwa
vikali na Rais Obama kuwa hawaamini hata chembe Wapakistani na endapo
wakiwaeleza kuhusu oparesheni hiyo basi siku hiyo hiyo Osama ataamishiwa
sehemu nyingine.
Obama akapendekeza kuwa kama ikitokea makomando wao
wamekamatwa kabla hawajamaliza oparesheni yao basi Admiral McRaven
atatakiwa ajiandae kumpigia simu Mkuu wa Majeshi Pakistani Ashfaq Parvez
Kayani kumshawishi kuwaachia makomando hao wa Marekani.
Lakini pia Obama akamuagiza Admiral McRaven awaandae
makomando wake kwa mapambano ya kijeshi kama ikitokea wamepewa upinzani
na wanajeshi wa Pakistan na hawataki kuwaruhusu waondoke.
Watu wote waliohudhuria kiako hicho cha kamati ya usalama
wakakubaliana na mpango huo wa kuvamia makazi ya Bin Laden kwa kutumia
helikopta isipokuwa Makamu wa Rais Joe Biden pekee aliupinga mpanga huo
kwa asilimia zote.
Licha ya Makamu wa Rais kuupinga mpango huo, siku ya tarehe
19 April kamati ya Usalama wa Taifa ilipokutana tena Rais Obama akatoa
idhini ya awali kukubali oparesheni hiyo itekelezwe. Na ikapewa jina
Oparesheni Neptune Spear.
Kesho yake McRaven pamoja na kikosi chake cha SEALs
wakaondoka marekani kuelekea Afghanistan ambapo walitumia takribani wiki
mbili kufanya mazoezi kuhusu oparesheni waliyoenda kuifanya.
Kikosi hiki kilifikia katika kambi ya Bagram nchini
Afghanistan na hapo palitengenezwa mfano wa nyumba kama ile
inayosadikiwa kumuhifadhi bin laden na kikosi cha SEALs wakafanya
wazoezi ya kutosha jinsi watakavyotekeleza zoezi hilo.
Ilipowadia siku ya tarehe 29, Rais Obama alimpigia simu
Kamanda McRaven kumuuliza juu ya maendeleo ya maandalizi. Pia akamuuliza
kama alikuwa na angalau ya chembe ya shaka kuhusu kufanikiwa kwa
oparesheni hiyo na kama alikuwa na shaka yoyote basi oparesheni hiyo
itahairishwa. McRaven akamjibu kuwa vijana wake wako tayari kwa
kutekeleza Oparesheni.
Obama akawapa idhini ya mwisho kuwa amewaruhusu kufanya oparesheni hiyo siku itakayofuata yaani tarehe 30 April.
Kesho yake Obama akataarifiwa kuwa oparesheni imehairishwa
kwa muda wa siku moja kutokana na hali ya hewa kutokuwa rafiki na badala
yake itafanyika kesho yake tarehe 1.
Jioni ya siku hiyo Obama akampigia simu tena McRaven
kumtakia kilala kheri yeye na makomando wake wa SEALs na akwashukuru kwa
kujitoa kwao kwa ajili ya Taifa lao.
Siku ya tarehe 1 May ilipowadia wajumbe wa kamati ya
usalama wa taifa walikusanyika katika chumba maalumu cha ikulu ya
marekani (situation room) kufuatilia oparesheni hiyo kupitia kwenye
runinga iliyokuwa inaonyesha picha za moja kwa moja zilizokuwa
zinachukuliwa ndege ya kujiendesha (drone) iliyokuwa inafuatilia tukio
zima la oparesheni hiyo.
Usiku wa manane Makomando wa SEALs wapatao 79 waliruka na
helikopta za kijeshi kutokea kambi ya kijeshi ya Bagram mpaka eneo la
mpakani Jalalabad. Walipofika hapo wakagawana. Makomando wapatao 24
pamoja na mbwa aina ya Belgia Malinois aliyeitwa Cairo waliingia kwenye
helikopta mbili aina ya Black Hawk ambazo zimeboreshwa kuzuia kuonekana
na Rada ya adui na kutotoa sauti.
Makomando waliosalia waliingia kwenye chopa kubwa za kijeshi aina ya Chinook.
Makomando ambao walipanda kwenye chopa za kivita aina ya
Black Hawk hawa ndio walipewa jukumu la kuvamia makazi ya Bin Laden.
Makomando wengine ambao walipanda kwenye chopa kubwa za kivita aina ya
Chinook hawa watakaa maili kadhaa kutoka eneo la tukio kama tahadhali
ikitokea wenzao wakahitaji msaada zaidi.
Baada ya kujigawanya hivi safari ya kuelekea kwenye makazi ya siri ya Bin Laden ikaanza.
Baada ya kuyafikia makazi ya Bin Laden Chopa moja ilitua
eneo la mbele ya jengo na nyingine ilitua nyuma kwa juu na makomando
wakashuka kwa spidi ya haraka kwa kutumia kamba.
Chopa ambayo ilitua mbele ya jengo, rubani aliiweka chini
kwa makosa kidogo na kusababisha mkia wa helikopta kugonga uzio wa ukuta
wa nyumba na almanusuura ipinduke chini juu lakini kwa ustadi akaiweka
sawa na makomando wakashuka salama ingawa helikopta tayari ilikuwa
imeharibika.
Baada ya makomando wote kufanikiwa kuingia ndani ya uzio
wakaanza kuisogelea mlango mkubwa wa nyumba. Pembeni ya nyumba kubwa
kulikuwa na vyumba vichache vimejengwa kwa ajili ya wageni na ndani yake
walitokea wanaume wawili waliokuwa na bunduki aina ya AK-47 na
kuwafyatulia risasi makomando wa SEALs.
Kabla watu hao hawajaleta madhara yoyote makonmando wa
SEALs waliwadondosha chini kwa risasi mbili kila mmoja. Watu hawa wawili
walikuja kutambulika baadae kuwa ni Abu Ahmed al-Kuwait pamoja na kaka
yake aliyeitwa Abrar.
Kisha makomando wakaingia ndani ya nyumba. Na baada ya
kuingia ndani kuna kijana akaonekana akikimbia kupandisha ngazi kwenda
ghorofa ya juu. Naye akadondoshwa chini kwa risasi. Kijana huyu naye
alikuja kutambulika kama mtoto mkubwa wa kiume wa Osama Bin Laden.
Baada ya kijana huyo kupigwa risasi mlango wa chumba
kilichopo ghorofa ya juu ulionekana kufunguliwa na mtu akachungulia. Pia
naye akafyatuliwa risasi kadhaa zikamkosa lakini moja ikampata ubavuni.
Mtu huyo aligeuka haraka na kurudi ndani chumbani lakini kabla
hajaufunga mlango wa chumba vizuri komando wa SEALs alifanikiwa kuruka
na kubiringika mpaka ndani ya chumba hicho.
Katika kujitahidi kujificha mtu huyo (Bin Laden) alimnyakua
mwanamke mmoja aliyekuwepo humo chumbani (mkewe Mdogo) na kumsukumia
kwa komando wa SEALs lakini komando alifanikiwa kumkwepa mwanamke huyo
na akafanikiwa kufyatua risasi iliyompata Osama kwenye paji la uso.
Papo hapo komando mwingine naye alikuwa ameshaingia
chumbani naye akafyatua risasi iliyompata Osama kifuani. Bin laden
akadondoka chini na komando mmoja akamfyatulia risasi nyingine kifuani
akiwa hapo hapo chini. Pale pale roho ya Osama Bin Laden ikaach mwili.
Komando mmoja akatoa simu ya mawimbi ya kijeshi na
kuwasiliana na kamanda McRaven aliyekuwa amebaki kwenye kambi ya Bagram.
Baada ya kupokea tu simu komando akamueleza kamanda wake kwa kifupi tu
"Geranimo".
Kamanda wake nae akaitafsiri taarifa hii kwa watu waliopo
Ikulu marekani pamoja na Rais Obama wakifuatilia Kupitia Satelaiti,
kamanda McRaven akawaeleza "For God and for the country, Geranimo
Geranimo Geranimo" kisha akamalizia "Geranimo EKIA" (EKIA - Enemy Killed
In Action (Aduai ameuawa kwenye mapambano)). Geranimo ndio lilikuwa
jina la fumbo (code name) la kumtambua Osama Bin Laden katika oparesheni
hii.
Seneta Hillary Clinton kipindi akiwa kama waziri wa mambo
ya nje wa Marekani naye siku alikuwepo Ikulu ndani ya situation room
anaeleza kuwa mara baada ya Rais Obama kusikia taarifa hii kwa msisimko
na hisia kubwa akaongea maneno machache tu, "we got him"
("tumempata/tumemmaliza").
Baada ya kutoa taarifa hiyo kuwa wamefanikiwa kumuua Bin
Laden, makomndo wa SEALs wakawakusanya wanawake na watoto wote
waliowakuta ndani ya nyumba hiyo na eakawafunga kwa pingu za plastiki na
kuwaacha hapo hapo. Kisha wakaubeba mwili wa Bin Laden na kuupakia
kwenye Chopa.
Lakini kabla ya kuondoka wakailipua ile chopa iliyopata
itilafu kwani isingeweza kuruka tena na hawakutaka watu wajue teknolojia
yao ya siri inayotumika kwenye chopa hizo.
Zoezi lote hili lilipangwa kutumia dakika 40, lakini kutoka
na umahiri wa hali ya juu wa makomando wa SEALs liliisha ndani ya
dakika 30 pekee. Risasi 16 tu ndizo zilifyatuliwa na watu 5 waliuwawa
(Osama, mtoto wake wa kiume, Abu Ahmed al-Kuwait, Abrar (kaka wa
al-kuwait), na mke wa Abrar).
Baadaya ya hapo wakaruka mpaka kambi ya Bagram kisha mwili
wa Bin laden ukapakiwa tena kwenye chopa na kupelekwa kwenye manowari ya
kivita ya NAVY iliyoko baharini. Huko sampuli za DNA zikachukuliwa na
mwili ukapigwa picha. Baada ya hapo mwili ukavilingishwa shuka jeupe
alafu ukatumbukizwa kwenye mfuko mkubwa na imara, vikawekwa na vyuma
vizito ndani yake, mfuko ukafungwa, ukatumbukizwa baharini. Huo ukawa
mwisho wa Bin laden Duniani.
HOTUBA YA UTHIBITISHO
Jioni ya siku hiyo Rais wa marekani Barack Obama alitoa hotuba ambayo itakumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo. Alisema;
"Habari za jioni, usiku huu napenda kuwataarifu Wamarekani
na Ulimwengu wote kuwa Marekani imeendesha oparesheni iliyofanikiwa
kumuua Osama Bin Laden kiongozi wa Al Qaeda na Gaidi anayehusika na vifo
vya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia......"
Ulimwengu ulisimama kwa sekunde kadhaa na wengine
hawakuamini masikio yao na mpaka sasa wapo wasio amini na kumeibuka
nadharia nyingi mno. Lakini hiki nilichokisimulia ndicho wanachoamini
CIA na serikali ya Marekani, kuwa siku ya Tarehe 1 mwezi May mwaka 2011;
"Geranimo E.K.I.A..... Adui aliuwawa katika mapambano."
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni