Watu wanne wameuwawa Jumamosi (12.11.2016) katika mripuko uliotokea
ndani ya kambi kubwa kabisa ya kijeshi ya Marekani nchini Afghanistan na
kujeruhi wengine kumi na nne ambapo utaifa wao haukuweza kufahamika
mara moja.
Kundi la Taliban limedai kuhusika na mripuko huo uliotokea
ndani ya kambi ya kikosi cha anga ya Bagram kaskazini ya mji mji mkuu wa
Kabul yenye ulinzi mkali wakati waasi wa kundi hilo wakizidisha
mashambulizi yao nchini kote kabla ya kuanza kwa kipindi cha majira ya
baridi ambapo kwa kawaida mashambulizi yao hupunguwa.
Msemaji wa
gavana wa jimbo la Parwan Waheed Sediqi ambako ndiko ilipo kambi hiyo ya
Bagram amesema mripuko huo umesababishwa na mtu aliyejitolea muhanga
ambaye amejiripua karibu na eneo la huduma ya chakula ndani ya kambi
hiyo.
Sediqi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba bado
hawajui utambulisho wa wahanga lakini mshambuliaji ni mmojawapo wa
wafanyakazi wa hapo.
Marekani ina takriban wanajeshi 10,000
nchini Afghanistan ambapo kikosi kikubwa kiko katika kambi hiyo ya
Bagram. Shambulio hilo linaonyesha ikiukaji mkubwa wa taratibu za
usalama ndani ya mojawapo ya vituo vya kijeshi vyenye ulinzi mkubwa
kabisa nchini Afghanistan.
Taliban yadai kuhusika
Kamanda
mkuu wa Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Afghanistan John
Nicholson ametowa rambi rambi kwa familia na marafiki wa wahanga
waliopoteza maisha yao katika shambulio hilo na kuwahakikishia kwamba
jamaa zao waliojeruhiwa wanapatiwa huduma nzuri kabisa na wataendelea
kuzingatiwa mawazoni.
Msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah
Mujahid amesema kundi hilo la waasi limehusika na shambulio hilo ndani
ya kambi ya Bagram na kudai kusababisha maafa makubwa kwa wanajeshi
wavamizi wa Marekani.Kambi hiyo ya Bagram imekuwa ikishambuliwa mara kwa
mara na waasi wa kundi hilo la Taliban.
Mwezi wa Disemba mwaka
jana mshambiliaji wa kujitowa muhanga wa kundi la Taliban aliyekuwa
akiendesha piki piki aliuwa wanaheshi sita wa Marekani karibu na kambi
hiyo hilo likiwa mojawapo ya shambulio lililosababisha maafa makubwa
dhidi ya vikosi vya kigeni nchini humo kwa mwaka 2015.
Kuongezeka mashambulizi
Shambulio
hili la Jumamosi linakuja baada ya lori lilosheheni mabomu kubamizwa na
ubalozi mdogo wa Ujerumani katika mji wa Mazar-i-Sharif kaskazini mwa
Afganistan hapo Alhamisi usiku na kuuwa takriban watu sita na kujeruhi
wengine zaidi ya 100.
Kuongezeka kwa mashambulizi hayo dhidi ya
vituo vya mataifa ya magharibi kunakuja siku chache tu baada ya
kumalizika kwa uchaguzi wa rais wa Marekani uliokuwa na ushindani mkali.
Suala
la Afghanistan lilikuwa halikupewa uzito wakati wa kampeni za uchaguzi
nchini Marekani juu ya kwamba hali nchini humo inaweza kuwa suala la
dharura kwa rais mpya wa Marekani.
Rais mteule wa Marekani
anatarajiwa kurithi vita vya Marekani vilivyochukuwa muda mrefu kabisa
na havina dalili ya kumalizika hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni