Baadhi ya makumpuni makubwa ya kigeni yaliyowekeza nchini Tanzania
huenda yakafikiria kupunguza au kusitisha shughuli zake kwa sababu ya
masharti magumu yanayowekwa dhidi ya makampuni hayo, ikiwemo kodi kubwa.
Kwa
mujibu wa mahojiano yaliyofanywa na shirika la habari la Reuters pamoja
na wakurugenzi wakuu wa makapuni ya kigeni yaliyowekeza nchini
Tanzania, kiasi ya makampuni sita yanafikiria mipango mipya kuhusu
uwekezaji katika sekta ya madini, mawasiliano ya simu au usafirishaji
kwa kutumia meli. Hiyo yote inatokana na juhudi zinazofanywa na Rais wa
Tanzania, John Magufuli kuubadili uchumi wa nchi hiyo.
Makampuni
matatu yamesema huenda yakapunguza shughuli zake za uwekezaji kwenye
taifa hilo la Afrika Mashariki, huku makampuni mengine mawili yakisema
yanafikiria kutanua zaidi shughuli zake katika nchi jirani na kampuni
moja imesema inaandaa mchakato wa kujiondoa kabisa nchini Tanzania.
Makampuni hayo yaliombwa kutotajwa majina kwa sababu ya umuhimu wa suala
hili na kwa sababu mipango yao hiyo bado haijatangazwa hadharani.
Kampuni
moja bado haijatoa msimamo wake jinsi ya kukabiliana na mageuzi hayo ya
serikali ya Tanzania, huku makampuni matano yakisema kuwa mipango yao
haikuathirika na mageuzi hayo, ikiwemo miradi miwili mikubwa, ule wa
kiwanda cha kusindika gesi asilia-LNG wenye thamani ya Dola bilioni 30
na mradi wa kiwanda cha mbolea wenye thamani ya Dola bilioni 3.
Tanzania na uwekezaji wa kigeni
Tanzania
inategemea zaidi uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja, kuliko nchi
nyingine za ukanda huo, kutokana na ukubwa wa uchumi wake. Mwaka
uliopita nchi hiyo ilipokea zaidi ya Dola bilioni 1.5, kwenye uchumi
ambao thamani yake ilikuwa chini ya Dola bilioni 45. Hiyo ni kwa mujibu
wa takwimu za Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Umoja wa Mataifa
pamoja na Benki ya Dunia.
Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye
amepewa jina la utani ''Tingatinga'' kutokana na miradi yake ya
miundombinu na aina ya uongozi wake, alizindua mchakato wa mageuzi yake
ya kiuchumi, baada ya kuchaguliwa kuiongoza nchi hiyo mwaka uliopita,
akiahidi kuubadilisha uchumi wa nchi hiyo, kuondoa urasimu na rushwa
pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi.
Mwaka huu serikali
ya Magufuli iliongeza kodi katika utumaji wa fedha kwa kutumia simu za
mkononi, mabenki, huduma za utalii na zile za usafirishaji wa mizigo.
Kodi ya mapato kwa mwaka wa fedha 2014/2015 jumla ilikuwa Shilingi za
Tanzania trillioni 9.8 ambazo ni sawa na Dola bilioni 4.5. Kwa mwaka wa
fedha 2016/2017, serikali ina lengo la kukusanya kodi ya mapato zaidi ya
trilioni 15.1, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Adolf Mkenda, amesema
wameyasikia malalamiko yanayotolewa na milango iko wazi, lakini
wanahakikisha kuwa kila mtu analipa kodi anayopaswa kulipa kwa
kuzingatia haki. Amesema lazima kuwepo na mageuzi mapya ambayo ni
magumu, ili kuufanya uchumi kuwa imara.
Mkurugenzi wa Huduma na
Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Richard Kayombo
amesema ongezeko la kodi ya mapato lilihitajika kwa ajili ya kulipia
miundombinu mipya nchini humo. Makampuni makubwa ya kigeni ambayo
yamewekeza nchini Tanzania ni pamoja na yale ya nishati, uhandisi,
mawasiliano ya simu, madini, na usafirishaji kwa kutumia meli.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni