Mkuu wa baraza jipya la utawala Burkina Faso alisema Rais na Waziri
Mkuu wapo salama chini ya ulinzi wa jeshi na karibuni wataachiwa.Brigedia Jenerali, Gilbert Diendere alizungumza na Sauti ya Amerika hapo Alhamis, siku moja baada ya wanajeshi kuiangusha serikali ya muda kwenye taifa la Afrika magharibi na kuwakamata viongozi wake. Jenerali huyo alisema jeshi lilipanga mapinduzi kwa sababu utaratibu wa kisiasa nchini humo haukuwa wa haki.
Alisema ataanza mashauriano ya kisiasa yanayojumuisha pande zote. Burkina Faso ilipanga kufanya uchaguzi wa urais na bunge hapo Oktoba 11. Tarehe hiyo hivi sasa ipo njia panda.
Watu wasiopungua watatu waliripotiwa kuuwawa wakati waandamanaji vijana walipojaribu kukusanyika karibu na makazi ya rais huko Ouagadougou na ubalozi wa Marekani ulisema vizuizi vya barabarani vimewekwa kote mjini humo.
White House mjini Washington ililaani vikali kile ilichokiita jaribio ambalo ni kinyume cha katiba la kuchukua madaraka. Naibu msaidizi wa Umoja wa Afrika, Erastus Mwencha aliwataka Alhamis viongozi hao wa kijeshi haraka kukabidhi madaraka kwa serikali ya muda. “Serikali yeyote ambayo haifuati katiba inalaumiwa moja kwa moja kwa sababu tunaamini katika utawala wa sheria na mabadiliko yeyote ya madaraka lazima yafuate utaratibu wa katiba”, alisema Mwencha.
Pia aliwasihi watu kutoshirikiana na jeshi kuchukua madaraka.
Serikali ya muda ilichukua madaraka nchini Burkina Faso wakati ghasia maarufu zilizomuondoa Rais Blaise Compaore madarakani mwezi Oktoba mwaka jana baada ya kuwepo mamlakani kwa miaka 27. Alipanga kubadili katiba ili aweze kuongeza utawala wake.

Wasiwasi wa taasisi za kimataifa na za nchini Yemen kuhusu jinai za ukoo
wa Aal Saud nchini humo umeongezeka mno hivi sasa huku Saudia na kundi
lake la nchi zinazotenda jinai, zikizidisha ukatili wao dhidi ya
wananchi wasio na ulinzi wa Yemen. Jeremy Hopkins, mjumbe wa Mfuko wa
Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF nchini Yemen ametoa tamko kuhusu
kuongezeka jinai na uvunjaji wa haki za wananchi wa Yemen na kuharibiwa
miundombinu ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu, na kusema kuwa, ana
wasiwasi mkubwa wa kutofika shehena ya misaada ya kibinadamu kwa watu 11
elfu waliokwama huko kusini mwa mji mkuu wa Sana’a, kutokana na
mashambulizi ya kikatili ya Saudia. Jeremy Hopkins ameongeza kuwa,
kitendo cha wanajeshi wa Saudia cha kushambulia shehena za misaada ya
kibinadamu na maeneo ya kusafishia maji nchini Yemen kinasikitisha sana
na kimewasababishia matatizo makubwa wakazi wa eneo hilo. Wizara ya Afya
ya Yemen jana Jumamosi ilitoa taarifa na kusema kuwa hospitali za mji
mkuu Sana’a hazina uwezo tena wa kupokea majeruhi na zimekumbwa na uhaba
mkubwa wa madawa, mafuta na mahitaji mengine ya lazima. Wizara ya Afya
ya Yemen imezitaka taasisi za kimataifa kuchukua hatua za haraka za
kuwaokoa wagonjwa na majeruhi wa mashambulio ya anga ya Saudia. Muhammad
al Masouri, Katibu Mkuu wa taasisi ya masuala ya kisheria ya “al Bayt
al Qanuni” ya Yemen amesema kuwa, hivi sasa haiyumkiniki tena kuzalisha
maji safi nchini humo kutokana na kukatika umeme na kuharibiwa mabomba
ya mafuta. Ametahadharisha kuwa, wananchi milioni 27 wa Yemen
wanakabiliwa na hatari kutoka kila upande. Wanajeshi wa utawala wa ukoo
wa Aal Saud jana Jumamosi pia waliendelea kufanya jinai kwenye maeneo ya
makazi ya raia katika mikoa ya Sana’a, Sa’ada, Taez, al Baydha na al
Hudaydah nchini Yemen na kuua makumi ya wananchi wasio na hatia kujeruhi
wengine 100. Vile vile ndege vamizi za Saudia na genge lake
zimeshambulia mara 20 majengo ya Wizara ya Vijana, Wizara ya Mambo ya
Ndani na kituo cha polisi huko Sana’a. Amma cha kusikitisha zaidi ni
kuona kuwa jinai hizo za Saudi Arabia zinafanyika mbele ya macho ya
jamii ya kimataifa na mashirika yanayojigamba kuwa ni watetezi wa haki
za binadamu na utawala wa sheria, ulimwenguni. Kimya cha mashirika hayo
kimezidi kuwa kikubwa katika hali ambayo, shirika la habari la al Ahd la
nchini Yemen limeripoti kuwa, Saudi Arabia inatumia pia makombora yenye
gesi ya sumu dhidi ya wananchi wa Yemen. Kwa mujibu wa shirika hilo,
gesi hizo za sumu zilizoenea kwenye makazi ya raia na mashamba ya
kilimo, zimepelekea kuzuka magonjwa ya ajabu nchini Yemen.









