Leo ni miaka mitano tangu kuuawa kwa
kiongozi wa muda mrefu wa Libya, Muammar Gaddafi ambaye alituhumiwa na
nchi za Magharibi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa ukatili
na kukandamiza wapinzani.
Utawala wake uliangushwa kufuatia
mashambulio ya ndege za kivita za nchi za Magharibi chini ya mwavuli wa
shirika la kujihami la Nato.
Baada ya kuuawa kwake, maelfu ya watu walishangilia kote nchini Libya.
Lakini
kadiri miaka ilivyosonga, watu wameanza kumkumbuka na kumuenzi hasa
baada ya taifa la Libya kutumbukia katika misukosuko ya kisiasa na vita.
Maelfu
ya watu wamekuwa wakitumia taifa hilo kujaribu kufika Ulaya, baadhi
wakifariki katika bahari ya Mediterranean. Mataifa ya Ulaya pia
yanalalamikia ongezeko la wahamiaji.
Katika nchi za Afrika, wakazi
wa nchi ambazo Kanali Gaddafi kwa njia moja au nyingine alichangia
kisiasa au kwa miradi ya ujenzi, anakumbukwa.
Mfano nchini Ghan
Karim Mohamed, 46, ambaye ni fundi wa nguo alisema Gaddafi alikuwa kama "masihi wa Afrika".
Alikuwa ameishi Libya wakati wa utawala wa Gaddafi.
"Nchini Libya, kila mtu alikuwa na furaha," anasema.
"Nchini
Marekani, kuna watu wanaolala chini ya madaraja. Lakini Libya hilo
halikufanyika. Hakukuwa na ubaguzi, hakukuwa na shida, hakuna
lililokosekana. Kazi ilikuwa nzuri na kulikuwa na pesa pia. Maisha yangu
yako yalivyo sasa kwa sababu ya Gaddafi. Alikuwa masihi wa Afrika."
Jake Wallis Simon alikutana na wanaume wengine wawili ambao pia waliunga mkono Karim.
Ndege moja ya Libya iliyoripotiwa kutekwa nyara ikiwa kwenye safari ya ndani mwa nchi imetua nchini Malta.
Ndege hiyo aina ya Airbus A320 ya shirika la ndege la serikali ya Libya, Afriqiyah, ilikuwa na abiria 118 wakati ilitekwa.
Watekaji nyara wawili waliripotiwa kutishia kuilipua ndege hiyo.
Ndege
hiyo ilikuwa safarini kutoka mji wa Sebha kusini magharibi mwa Libya
ikielekea mji mkuu Tripoli kabla ya kuelekezwa nchini Malta, kwa mujibu
wa shirika la habari la Reuters.
Karibu watu wote waliokuwa ndani ya ndege wanaripotiwa kuondoka.
Watekaji nyara hao waliondoka ndani ya ndege hiyo na kujisalimisha.
Mmoja
wao alikimbia kituo kimoja cha runinga nchini Libya kuwa yeye ni mkuu
wa chama chama kinachompendelea kiongozi wa zamani wa Libya Muammar
Gaddafi.
Meya wa mji wa Sebha nchini Libya ambapo ndege hiyo
ilikuwa ikitokea anasema kuwa watekaji nyara hao wanatafuta hifadhi ya
kisiasa.
Rais wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli amemteua Prof Yunus Mgaya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) saa chache baada ya
kumfuta kazi mkurugenzi wa awali Dkt. Mwele Malecela.
Taarifa kutoka ikulu imesema uteuzi wa Prof Mgaya unaanza mara moja.
Dkt Mwele Malecela, alifutwa kazi siku moja tu baada yake kutangaza kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.
Taarifa
ya kufutwa kwake, iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya ikulu
Gerson Msigwa, haikueleza sababu ya kufutwa kazi kwa Dkt Malecela,
Hata
hivyo, kulikuwa kumetokea habari za kukinzana kutoka kwake na wizara ya
afya kuhusu kuwepo kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.
Alitangaza
kuwepo kwa virusi hivyo nchini Tanzania siku ya Alhamisi lakini Ijumaa,
baada ya habari hizo kuenea kwenye vyombo vya habari, waziri wa afya
Ummy Mwalimu akatoa taarifa kukanusha habari hizo.
Dkt Mwele
Malecela alikuwa ametangaza kwamba virusi hivyo vimepatikana mkoani
Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na Mkoani Geita, kaskazini magharibi
mwa Tanzania.
Kwa mujibu wake, virusi hivyo viligunduliwa wakati wa
utafiti uliofanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira
yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.Kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti huo, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi vya Zika.
Hata hivyo wizara afya nchini humo, ilitoa taarifa ambapo inakanusha kuwepo kwa virusi hivyo.
"Kama
nilivyoeleza mnamo Februari 2016, ugonjwa huu bado haujaingia nchini,
na leo pia napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa Tanzania
haujathibitishwa kuwepo na ugonjwa wa Zika," taarifa ya wizara ya afya
imesema.
Wizara hiyo inasema uchunguzi uliofanywa na NIMR ulikuwa
wa kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya Zika na
Chikungunya.
"Matokeo haya bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina
zaidi kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani,"
wizara ilisema.
Asili ya Zika
Jina la virusi hivyo linatokana na msitu wa Zika, Uganda ambapo virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza 1947.
Wengi
wa walioambukizwa aina ya awali ya virusi walikuwa wakipatwa na homa
ambayo si kali sana, mwasho na maumivu katika maungio.
Makamu wa rais nchini Afrika Kusini, Cyril
Ramaphosa, ametangaza kwa mara nyingine tena kuwa yuko tayari kumrithi
rais Jacob zuma kwenye uongozi wa chama cha ANC. Ndani ya mwaka mmoja, chama cha ANC kitamchagua kiongozi wake, ambaye atakiwakilisha katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2019.
"Niko tayari kukitumikia chama
cha ANC," alisema Cyril Ramaphosa Jumatano hii Desemba 14 kwenye redio
moja nchini Afrika kusini. Hii ni mara ya pili ndani ya muda wa wiki
ambapo Makamu wa rais anasema kuwa tayari kuchukua uongozi wa chama cha
ANC (African National Congress).
Cyril Ramaphosa alisema kuwa anaendelea kuyasikiliza matawi
mbalimbali ya chama cha ANC, akitangaza kwamba atafurahi kama atapata
uungwaji mkono.Kwa kawaida Makamu wa rais anatakiwa kumrithi rais wake,
lakini Cyril Ramaphosa anakwenda kwa tahadhari. Anajua kwamba kumrithi
ni vigumu, kwa sababu chama cha ANC kimegawanyika kati ya wanaomuunga
mkono Jacob Zuma na wale wanaompinga.
Ili kuchukua nafasi ya rais anayeshirikiana naye tangu mwaka 2012
kama kiongpzi wa chama cha ANC, Cyril Ramaphosa atapambana na mgombea
mwenye ushawishi mkubwa nchini Afrika Kusini, ambaye ni Nkosazana
Dlamini-Zuma, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika na mke wa zamani wa
rais Zuma.
Bado hajatangaza rasmi kuwania katika uchaguzi wa urais, lakini
tayari anaonekana kufanya hivyo kwa sababu anaungwa mkono na wanaounga
mkono Zuma. Nkosazana Dlamini-Zuma pia anawachukulia miongoni mwa
washirika wake vijana na Wanawake wa chama cha ANC pamoja na jimbo la
KwaZulu-Natal ambapo anazaliwa rais Jacob Zumaya rais. Rais wa Afrika
Kusini, mwenyewe anaweza pia kumuunga mkono.
Upinzani nchini Gambia wasema Endapo rais
anayemaliza muda wake nchini humo Yahya Jammeh atakataa kuondoka
Madarakani atachukuliwa kama muasi. Yahya Jammeh alirejelea kauli yake
hivi karibuni baada ya kutambua ushindi wa mshindani wake Adama barrow,
na kutaka kura zirudi kuhesabiwa upya.
Katikati mwa juma lililopita
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Afrika Magharibi, Mohamed Ibn
Chambas, alisema kuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh anapaswa "kuwa tayari
kukabidhi madaraka" ifikapo mwezi Januari mwakani.
Bw ibn Chambas alisema Umoja wa Mataifa hautaendelea kufumbia macho
viongozi ambao hushindwa na kisha baadaye wanatumia nguvu kwa kuchukua
madaraka.
"Upinzani ulishinda uchaguzi, ambao uliku halali" amesema Mwakilishi
Maalum wa Katibu Mkuu wa wa Ban Ki-moon katika Afrika ya Magharibi.
Jumanne Desemba 13 Marais wanne kutoka Afrika Magharibi walifanya
ziara katika mji mkuu wa Gambia, Banjul na kujaribu kumshawishi Yahya
Jammeh kukubali kushindwa katika uchaguzi wa urais na kukabidhi
madaraka, bila mafanikio.
Mihula ya miaka mitano ya Bw Jammeh itamalizika Januari 19, Mohamed
Ibn Chambas amesema, huku akiongeza kuwa "atakuwa tayari kukabidhi
madaraka" tarehe hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameendelea kulaani
hatua ya jeshi kudhibiti Tume ya Uchaguzi na kuwafukuza wafanyakazi
wote ambao kwa sasa hawawezi kwenda kazini.
Awali Ban Ki-moon alimtaka rais Jammeh kuamuru wanajeshi hao kuondoka katika tume hiyo mara moja.
Upinzani nchini Gambia umemuonya Yahya Jammeh ikiwa atakaidi kuachia ngazi, kuwa atachukuliwa kama adui wa nchi hiyo.
Papa francis anajaribu kutafuta suluhisho kwa mzozo wa kisiasa wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwaita viongozi wa kanisa walokua
wanaongoza juhudi za upatanishi kati ya serikali ya Joseph Kabila na
upinzani, juu ya hatua za kuchukuliwa baada ya muda wa Kabila wa
Jumatatu tarehe 19 unafika.
Mkuu wa Kanisa la Katholiki alichukua hatua hiyo baada ya viongozi wa
kidini kukutana na Rais Kabila siku ya Ijuma na kiongozi wa upinzani
Étienne Tshisekedi, bila ya kupata ufumbuzi.
Muungano wa upinzani wa "Ressmblemement" unampango wa kuitisha
maandamano Jumatatu ambayo Wakongo wengi na Jumia ya kimataifa wanahofu
yanaweza kuzusha ghasia nchini humo.
Inaripotiwa kwamba mazungumzo kati ya pande mbili yanatazamiwa kuanza tena siku ya Jumatano.
Kwa upande mwengine afisa wa juu wa Ressemblement anamhimiza Rais
Joseph kabila kufikia makubaliano na kundi hilo na kuacha madaraka ili
kuruhusu kipindi cha amani cha kukabiliana madaraka.
Muda rasmi wa mhula wa Kabila unamalizika jumatatu tarehe 19.
Freddy Mbuyamu Matungulu kiongozi wa kundi la Nabiso Kongo, "Kongo
Yetu", anasema viongozi wa mungano wa Ressemblement wanakutana Kinshasa
kuamua utaratibu wa mpito na hali ya baada ya muda wa Kabila kupita.
Wakili Benedict Ishamakaki anayemwakilisha mahakamani mkurugenzi
mtendaji wa Jamii Media ya nchini Tanzania, kampuni inayomiliki mtandao
wa Jamii Forum, Maxence Melo alisema mtazamo anaouona katika kesi ya
mteja wake ni kama anakomolewa.
Alipozungumza na Sauti ya Amerika-VOA
inayotangaza kutoka Washington DC, mwanasheria Ishamakaki alisema
ukiangalia chombo kilichomfungulia mashtaka mteja wake, katika barua
kutoka kwenye chombo hicho waliandika walikuwa wanasumbuka kumuandikia
barua Melo ili kupata taarifa Fulani, kwa maana hiyo kwa maoni yake
mwanasheria anaona kama ni “kulipizana kisasi kwamba wewe ulikuwa
unatusumbua kupata taarifa ngoja na sisi tukusumbue kupata dhamana”.
Pia aliongeza kuwa mazingira yaliyotengenezwa mahakamani siku ya
Ijumaa aliposomewa mashtaka na kupelekea mteja wake kukosa dhamana kwa
maoni yake anaona kama “wanachezewa mchezo Fulani”.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
inakabiliwa na hatari kubwa ya kutumbukia kwenye machafuko, Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa limetahadharishwa.
Mjumbe wa UN Maman
Sidikou amesema wanajeshi 18,000 wa kulinda amani wa umoja huo ambao
wamo nchini humo hawana uwezo wa kukabiliana na ghasia kama hizo iwapo
zitazuka.
Maandamano yenye umwagikaji wa damu yamekuwa
wakishuhudiwa mara kwa mara kufuatia hatua ya kuahirishwa kwa tarehe ya
uchaguzi wa rais.
Upinzani unamtuhumu Rais Joseph Kabila kwa kujaribu kukwamilia mamlaka hata baada ya kumalizika kwa muhula wake Desemba.
Watu
kadha walifariki wakati wa maandamano ya kupinga serikali mwezi jana
mjini Kinshasa baada ya tume ya uchaguzi kusema haingewezekana uchaguzi
ufanyike Novemba.
Makao makuu ya vyama vitatu vya upinzani yalishambuliwa na kuchomwa moto.
"Wadau
kutoka pande zote wanaonekana kuwa tayari zaidi na kutumia ghasia
kutimiza malengo yao," Bw Sidikou, mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha
UN kunachojulikana kama Monusco, aliambia baraza la usalama la UN
Jumanne.
Ingawa Monusco itafanya kila iwezalo kulinda raia, haina uwezo wa kukabiliana na hatari zote zilizopo."
Aliongeza:
"Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeingia kipindi cha hatari kubwa kwa
uthabiti wake. Kipindi kijacho kitakuwa kigumu sana, kuna uwezekano wa
kufikia pahala ambapo ghasia zitazidi."
DR Congo haijawahi kuwa na rais aliyekabidhi madaraka kwa njia ya amani kwa mrithi wake tangu uhuru miaka 55 iliyopita.
Bw Kabila aliingia madarakani 2001 baada ya kuuawa kwa babake Laurent Kabila.
Mwanzilishi wa Jamii Forums Maxence
Melo, ambaye amekuwa akizuiliwa na maafisa wa polisi nchini Tanzania
tangu Jumanne wiki iliyopita, amepewa dhamana na mahakama ya hakimu
mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Masharti ya dhamana ni wadhamini
wawili ambao wote walisaini bondi ya shilingi milioni 5 za Tanzania na
kwamba Maxenxe hatatoka nje ya Dar es Salaam pasipo kibali cha mahakama.
Bw Melo alishtakiwa kwa makosa matatu Ijumaa.
Makosa
hayo ni kuendesha na kumiliki tovuti ambayo haijasajiliwa nchini
Tanzania, na kuzuia uchunguzi wa polisi kwa mujibu wa Sheria ya Makosa
Kimtandao.
Hakuweza kuwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana Ijumaa na alizuiliwa gereza la Keko wikendi.
Kesi itasikilizwa tena tarehe 29 Desemba.
Kampuni ya mtandaoni ya Yahoo imesema Jumatano kuwa kuvuja kwa
taarifa mwezi Agosti 2013 kuliweka taarifa za zaidi ya watumiaji bilioni
moja kwenye hatari.
Kampuni ya mtandaoni wa Yahoo imesema Jumatano kuwa kutolewa kwa siri
taarifa hapo mwezi Agosti 2013 kuliweka taarifa za zaidi ya watumiaji
bilioni moja kwenye hatari. Yahoo imefafanua kuwa wizi huo wa mitandaoni
ni tofauti na uliofanyika Septemba wakati kampuni hiyo ilipofichua kuwa
taarifa za zaidi ya watumiaji milioni 500 zilivuja 2014.
Yahoo inaamini kuwa mtu asie na idhini Agosti 2013 aliiba taarifa
zinazohusina na zaidi ya watumizi bilioni moja wa mtandao huo. Taarifa
zilizoibiwa ni pamoja na majina ya watu, akaunti za barua pepe, nabari
za simu, siku za kuzaliwa pamoja na mswali ya kiusalama.
Taarifa kuhusu kadi za benki inaaminika kuwa hazikuvuja. Kampuni ya
Yahoo yenye makao yake Snnyville California inajiandaa kununuliwa na
kampuni ya Verizon kwa dola bilioni 4.8.
Ben Saanane
Sakata la kutoweka kwa afisa wa cheo cha juu wa chama cha Demokrasia
na Maendeleo CHADEMA, Ben Saanane limechukua sura mpya baada ya chama
hicho kutoa tamko rasmi kwamba hawajui alipo msaidizi huyo wa mwenyekiti
wa taifa CHADEMA,
Kupitia mwanasheria mkuu wake Tundu Lissu, chama hicho kimeitaka
serikali kupitia jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya mahali
alipo Ben Saanane, msaidizi wa mwenyekiti wa taifa upande wa siasa na
jamii, anayedaiwa kutoweka tangu Novemba 14 mwaka huu na mara ya mwisho
kupata taarifa zake inadaiwa aliwasiliana na mwenyekiti wa chama hicho
Freeman Mbowe.
Tundu Lissu amesema serikali ndio yenye ulinzi na
udhibiti mkubwa wa mipaka ya nchi ambapo inao uwezo wa kufahamu kama mtu
ametoka nje ya nchi au yupo ndani ya nchi hivyo wanawajibu wa kufanya
kila njia ya kumpata Ben Saanane ambaye taarifa za kutoweka kwake kwa
mara ya kwanza zilitolewa na ndugu zake wa karibu.
“Wakisema wamemkamata tutawauliza kwa nini wamemkamata na kumshikilia
muda wote. Hatumtuhumu mtu yoyote tutauliza masuala ambayo yanahitaji
kuulizwa. Huyu Ben Saanane kuna kipindi aliandikiwa barua ya kutishwa,”
alisema Lissu.
Katika hatua nyingine CHADEMA pia imetaka uchunguzi wa kutosha juu ya
maiti za watu zilizookotwa mto Ruvu ili kujiridhisha aina ya kifo chao
licha ya kwamba taarifa za awali zilidai watu hao ni wahamiaji haramu.
Lissu alisema,” Serikali kwa maana ya jeshi la Polisi wanatakiwa
kufanya inquest. Inquest ni uchunguzi wa sababu za kifo. Ilikujibu suali
hiki kifo kimesababishwa na jinai au ni kifo cha kawaida."
Akanongezea kufafanua kwamba,” wale wataalamu wa uchunguzi
(pathologists) lazima wafanye uchunguzi wakitaalamu kutambua huyu mtu
amekufa kwa sababu gani.”
Hata hivyo Mwandishi wa VOA Dina Chahali anasema maiti za watu saba
wasiojulikana ziliokotwa katika mto Ruvu mkoani pwani Desemba 11 mwaka
huu.
Taarifa za awali kutoka polisi zilieleza kwamba miili hiyo
inasemekana ni ya wahamiaji haramu, na tayari imezikwa. waziri mkuu
Kassim Majali katika maadhimisho ya Maulid hivi karibuni pia aliagiza
mamlaka husika kufanya uchunguzi wa vifo hivyo na kutoa taarifa kamili.
Kampuni za mitandao katika Jamuhuri
ya Kidemokrasia ya Congo zimeamrishwa kufunga mitandao ya kijamii
kwanzia Jumapili hii. Hii ni kwa mujibu wa shirika la habari AFP.
Mmoja
wa maafisa wa kampuni ya mtandao ameambia AFP kamba wamepokea amri hiyo
kutoka kwa serikali kubana mtandao wote. Muhula wa Rais Joseph Kabila
chini ya katiba unatarajiwa kumalizika Jumatatu ya wiki ijayo.
Wanaharakati
wameanzisha kampeini kwenye Twitter #ByeByeKabila, kama njiya ya
kumshinikiza kiongozi huyo kuachia ngazi. Chini ya katiba ya DRC Rais
Kabila alistahili kumaliza muhula wake Decemba mwaka huu na kufanyike
uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo tume ya uchaguzi ilisema haikuwa tayari
kuanda uchaguzi. Mazungumzo ya kitaifa ambayo yalisusiwa na vyama vikuu
vya upinzani yalipendekeza uchaguzi kuahirishwa hadi mwaka 2018, ambapo
Kabila ataongoza kipindi cha mpito.
Licha ya kwamba mahakama ya
kuu imeridhia makubaliano hayo, hata hivyo wapinzani wamesema lazima
Kabila aondoke madarakani kwanza na kuundwe utawala wa mpito bila yeye
kuongoza.
Rais huyo ameahidi kwamba hatagombea mwaka 2018, lakini
wapinzani wamepinga hilo. Kumekua na maandamano yaliokumbwa na ghasia
na vifo kushinikiza Joseph Kabila kuheshimu katiba ya nchi na kustaafu.
Katiba haimkubalii kuwania Urais tena baada ya kumaliza mihula miwili.
Binti wa Rais wa zamani nchini
Msumbiji, Armando Guebuza, Valentina Guebuza ameripotiwa kupigwa risasi
na kuuawa katika mji mkuu wa Maputo. Mumewe, Zofino Muiuane amekamatwa
na polisi kufuatia tukio hilo lililofanyika Jumatano.
Bi Guebuza
alikua na umri wa miaka 36 na imeripotiwa alipigwa risasi mara kadhaa
nyumbani kwake na kufariki dunia kutokana na majeraha wakati akipelekwa
hospitalini.Mumewe alikamatwa katika moja wapo ya maeneo ya burudani
mjini Maputo, kwa mujibu wa gazeti moja.
Valentina Guebuza
aliorodheshwa nafasi ya saba miongoni mwa wanawake chipukizi wenye
ushawishi Barani Afrika na jarida la Forbes mwaka wa 2013. Alishikilia
nafasi ya juu katika kampuni kadhaa za mawasiliano pamoja na biashara
zinazomilikiwa na familia.
Mumewe bwana Muiuane ni mfanyibiashara
na aliwahi kufanya kazi katika kampuni ya sigara ya 'British American
Tobacco'. Wawili hao walifunga ndoa mwaka wa 2014 kwenye sherehe
iliyohuhduriwa na wageni 1,700 akiwemo Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.
Mfalme wa Zwaziland Mswati wa Tatu na binti wa Rais wa Angola
Isabel dos Santos. Walijaaliwa na mtoto wa kike mwaka uliopita. Armando
Guebuza alistaafu kama Rais mwaka wa 2014 baada ya kuhudumu kwa mihula
miwili.
aarifa kutoka kwa Jamii Forums inasema Bw Melo alizuiliwa kwa kutotoa taarifa za watumiaji wa mtandao huo.
Alitarajiwa kufikishwa kortini Jumatano lakini hilo halikufanyika.
Badala
yake, polisi walifika afisi za Jamii Forums kufanya upekuzi kisha
wakawahoji wafanyakazi na kuchukua maelezo ya utendaji kazi wao.
Mashirika
ya kutetea haki za kibinadamu yanasema Melo anashikiliwa kinyume cha
sheria kwani sheria inataka mtu asishikiliwe na polisi kwa muda unaozidi
saa 24 bila kuwasilishwa kortini.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilitoa taarifa Jumatano kulaani kuendelea kuwekwa kizuizini kwa Bw Melo.
"Kituo
kinalitaka jeshi la polisi kuheshimu katiba ya Tanzania ya mwaka 1977
ibara ya 1977 inayotoa haki kwa kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu
huru," taarifa ya kituo hicho ilisema.
Kupitia taarifa, mratibu wa
kitaifa wa shirika la watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania
(THRDC) Bw Onesmo Olengurumwa aliwataka maafisa wa polisi kumwachilia
huru mara moja Bw Melo kwa sababu "wameshindwa kumfungulia mashtaka
kortini katika muda unaotakikana kisheria."
Aliitaka serikali
kuhakikisha Sheria ya Makosa ya Kimtandao haitumiwi kukandamiza uhuru wa
kujieleza katika mtandao nchini Tanzania.
Wakili wa Melo, Jebra
Kambole anasema Ijumaa wana mpango wa kuiandikia Mahakama Kuu ombi la
kuiomba iwalazimishe polisi kumpeleka Melo mahakamani hapo afunguliwe
mashtaka au aachiliwe
Katika mataifa 20, ambapo virusi hivyo vinaaminika kuchangia kuzaliwa
kwa watoto wenye vichwa vidogo, na hasa Brazil, tahadhari imetolewa.
Ni
mlipuko wa maradhi ambao unaendelea, na Dkt Anthony Fauci, ambaye ni
mtaalamu wa maradhi ya kuambukiza katika Taasisi ya Taifa ya Afya
Marekani.
Kuenea huku kwa kasi kwa virusi vya Zika ndiko kwa
karibuni zaidi kati ya magonjwa manne ya virusi yanayoenezwa na mbu
mataifa ya Magharibi katika kipindi cha miaka 20, anaandika Dkt Fauci
kwenye makala katika jarida la kimatibabu lathe New England Journal of
Medicine.
Mlipuko huu unafuata mlipuko wa maradhi ya kidingapopo
(homa ya dengue), virusi vya Nile Magharibi, na majuzi zaidi,
chikungunya. Sawa na maradhi haya, virusi vya Zika pia huenezwa na mbu.
Lakini kinyume na virusi hivyo vingine, hakuna chanjo dhidi ya Zika. Je, ni njia gani iliyopo ya kukabiliana na virusi hivi?
1. Kutumia dawa au mafuta ya kufukuza mbu
Ushauri
wa kwanza kabisa ni kuepukana na mbu. Kituo cha Kudhubiti na Kuzuia
Maradhi (CDC) nchini Marekani kinapendekeza watu wajipake mafuta yenye
kemikali za kufukuza mbu kama vile N, N-diethyl-meta-toluamide (DEET) au
picaridin.
Mafuta haya yanafaa kujipakwa mara kwa mara, kwa
kufuata maagizo kwenye mikebe, au mtu anapoanza kuumwa na mbu. Mtu
anafaa kujipaka baada ya kujipaka mafuta ya kukinga ngozi dhidi ya miali
ya jua.
Mafuta mengi ya kufukuza mbu ni salama hata kwa kina mama
waja wazito, lakini ni vyema kutafuta ushauri wa daktari kabla ya
kuanza kuyatumia.
2. Kuvalia mavazi ya kufunika mwili
Wataalamu
pia wanakubaliana kwamba inafaa kuvalia mavazi yanayofunika mwili
vyema. Mfano shati au nguo zenye kufunika mikono na pia suruali au
long’i ndefu. Mavazi yanafaa kuwa mazito kuzuia mbu kufikia ngozi.
Katika baadhi ya mataifa, mavazi huwekwa dawa maalum aina ya permethrin, ambao hufukuza mbu.
Iwapo utajipaka mafuta ya kufukuza mbu, usijipake na kisha kufunika maeneo uliyojipaka kwa nguo unazovalia.
3. Kuzuia mbu kuingia nyumbani
Ikiwezekana, wataalamu wanawashauri watu walale ndani ya nyumba zilizojengwa vyema na kuwekwa kinga ya kuzuia mbu kuingia.
Usiku, lala chini ya neti zilizotibiwa.
Lakini usitahadhari usiku pekee kwani mbu aina ya Aedes aegypti, wanaoeneza virusi vya Zika, hupenda sana kuuma watu mchana.
4. Chunga mimea inayokua ndani ya nyumba
Ingawa ni muhimu kuzuia mbu kuingia, ni muhimu hata haidi kuzuia mbu kuzaana. Na mbu huhitaji maji.
Watu
wanashauriwa kuchunga sana maeneo yenye maji yaliyosimama kwani huko
ndiko viluwiluwi wa mbu huwa. Maeneo haya ni pamoja na mikebe, maeneo ya
kuwapa mifugo na wanyama wengine lishe, jagi za kuweka maua, vibanda
vya kufugia ndege na mimea ya kupandwa ndani ya nyumba.
Ni vyema
pia kusafisha mifereji ya maji mara kadha kila wiki, mufunika matangi ya
mali na vidimbwi la sivyo kuweka dawa ya krolini (krolini huwafukuza
mbu).
Maji ambayo yametulia kwa zaidi ya siku tano yanafaa kutupwa
kwa kumwagwa ardhi kavu, kwani viluwiluwi wa mbu watafariki baada ya
maji kukauka. Kiasi kidogo tu cha maji kinatosha kwa viluwiluwi hao
kukua kwa hivyo, ni vyema kuosha na kukausha vyema maeneo hatari.
5. Kufunika taka
Maeneo ya kutupwa taka mara nyingi huwa na maji na hutumiwa sana na mbu kuzaana.
Ili kuzuia hili, ni vyema kufunika taka, hasa katika mifuko ya plastiki.
Tairi
kuukuu na vitu vingine vya ujenzi pia vinafaa kuwekwa vyema, kwani sana
huhifadhi maji ambayo yanaweza kutumiwa na viluwiluwi wa mbu.
6. “Kunyunyizia dawa”
Maafisa
nchini Brazil, ambako virusi vya Zika vimeenea sana, wanatafakari wazo
la kunyunyizia maeneo yaliyoathiriwa na virusi hivyo dawa ya kuua
mbu.Hii inachukuliwa kama njia ya dharura kabla ya michezo ya Olimpiki,
ambayo itaanza mjini Rio de Janeiro mwezi Agosti.
Hata hivyo, kuna utata kwani njia hii inaweza kuwa na madhara mengine kwenye mazingira na pia kuathiri afya ya wakazi.
7. Kudhibiti mbu
Serikali
katika nchi kadha za Amerika Kusini tayari wameanza kampeni ya
kuangamiza mbu wanaobeba virusi vya Zika kwa kutumia teknolojia.
Moja
ya njia tata zinazopendekezwa ni kueneza mbu waliofanyiwa mabadiliko ya
kijeneti ambao hawana uwezo wa kuzaana. Hili litapunguza idadi ya mbu
na kuzuia ugonjwa huo kuenea.
Wengine wamejaribu mbinu nyingine, mfano jiji la Itapetim nchini Brazil. Maafisa mjini humo wanatumia samaki kuangamiza mbu huo.
Samaki hao hula mayai ya mbu na hivyo kuzuia kuongezeka kwa idadi ya mbu hao.
8. Vifaa ya kukabili mbu nyumbani
Maafisa
wa serikali wanapojaribu kukabiliana na mbu kwa kiwango kikubwa, watu
binafsi manyumbani pia wanatumia njia mbalimbali kukabili mbu.
Wanatumia
vifaa mbalimbali vya kuwawinga na kuwaua mbu. Mfano ni kutumia kifaa
kinachoiga mwili na kutoa hewani ya kaboni dayoksaidi pamoja na joto,
ili mbu waingie ndani wakidhani ni binadamu.
Mitambo mingine ya
kunyunyiza dawa ya kuua mbu pia inatumiwa, lakini inapingwa na baadhi ya
watu kwani inaathiri pia nyuki, vipepeo na wadudu wengine.
9. Kukwepa kusafiri
Wale wanaoishi maeneo ambayo hayajaathirika na virusi hivyo, wanajizuia kusafiri.
CDC
imewashauri wanawake waja wazito nchini Marekani kuahirisha ziara zao
Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean kadiri wawezavyo.
Kituo hicho kimewashauri wanawake wanaopanga kusafiri maeneo hayo kutafuta ushauri wa madaktari kwanza.
Shirika la Afya Duniani (WHO), hata hivyo, halijaunga mkono ushauri huo wa CDC.
“Kwa
kutumia ushahidi uliopo, WHO haipendekezi vikwazo vya usafiri au
biashara kuhusiana na virusi vya Zika. Lakini kama tahadhari, mataifa
mbalimbali yanaweza kutoa mapendekezo mbalimbali ya kiafya na kuhusu
usafiri kwa raia wake, kwa kuzingatia utathmini,” WHO imesema.
0. Kuzuia kuenea
Mtu anapoambukizwa, hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa kuzuia kuumwa tena na mbu wiki ya kwanza baada ya kuugua, CDC inasema.
Hii
ni kwa sababu virusi vya Zika vinaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja
hadi kwa mtu mwingine kupitia damu baada ya kuumwa na mbu.
Ingawa
hatari ya kuenezwa kwa virusi hivi kupitia kujamiiana haijathibitishwa
kisayansi, baadhi wanapendekeza watu watumie mipira ya kondomu hadi wiki
mbili baada ya kupona.
Aidha, watu wachukue tahadhari kuepusha kuambukizwa virusi hivyo kupitia mate na majimaji ya mwili.
Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu, NIMR imethibitisha kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Mwele Malecela, virusi hivyo
vimepatikana mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na Mkoani Geita,
kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Utafiti huo ulifanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.
Kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti huo, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi vya Zika.
Dkt
Mwele Malecela ameambia BBC kwamba kwa sasa serikali inaangazia kuzuia
wajawazito wasiumwe na mbu ambao wanaaminika kueneza virusi hivyo.
"Bado
tunajaribu kuangalia ni aina gani ya virusi vya Zika. Lakini hiyo ni
dhahiri, tukizingatia kwamba mbu wanaoambukiza Zika wako nchini kwetu na
mazingira yaliyoko nchini kwetu hayatofautiani sana na yale ya Amerika
ya Kusini na nchi kama Thailand ambako ugonjwa huo unapatikana," amesema
Bi Malecela.
"Ugunduzi huu tumeupata kwa watu na tutaendelea
kufanya kazi kuangalia kama tutaupata kwa mbu ambao utatuhakikishia basi
kwamba ugonjwa huo ina maana umekuwepo nchini ni vile tu ulikuwa
haujaonekana."
"Heri nusu shari kuliko shari kamili, kulielewa
jambo na kujua kwamba lipo nchini na kujua kwamba wajawazito wanaweza
kuzaa watoto wenye matatizo haya kutatuwezesha kuzuia ugonjwa huyu.
Tutahakikisha nguvu zetu za kupambana na mbu wanaoeneza virusi hivi
zinaongezeka."
Virusi vya Zika zimekuwa vikisababisha watoto
kuzaliwa wakiwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo katika mataifa ya
Amerika Kusini na sana Brazil.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily News
la Tanzania, Dkt Malecela, alipokuwa akitangaza matokeo ya utafiti huo
mjini Dar es Salaam alisema uchunguzi wao ulionesha kati ya watoto 80
waliozaliwa wakiwa na matatizo ya kimaumbile, asilimia 43.8 walikuwa na
virusi vya Zika.
Mapema mwaka huu, serikali ya Tanzania iliwaagiza
madaktari wote kuwa macho kuhusu hatari ya virusi hivyo mlipuko
ulipotokea nchini Brazil.
Virusi vya Zika huenezwa sana na mbu ingawa kumeripotiwa pia visa vya watu kuambukizwa virusi hivyo kupitia kufanya mapenzi.
Haijabainika
iwapo aina ya virusi vya Zika vilivyopatikana Tanzania ni vile ambavyo
vimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo Amerika Kusini.
Virusi vya aina hiyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika katika visiwa vya Cape Verde mwezi Mei mwaka huu.
Jina la virusi hivyo linatokana na msitu wa Zika, Uganda ambapo virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza 1947.
Wengi
wa walioambukizwa aina ya awali ya virusi walikuwa wakipatwa na homa
ambayo si kali sana, mwasho na maumivu katika maungio.
Lakini kwa
aina ya sasa, ambayo mlipuko wake ulianza mwishoni mwa mwaka 2015 nchini
Brazil, dalili zake zimekuwa kali na virusi hivyo vinaaminika
kusababisha kudumaa kwa ubongo na kasoro nyingine mwilini.
1947: Wanasayansi wanaotafiti kuhusu homa ya manjano msitu wa Zika, Uganda wagundua virusi hivyo kwenye tumbili.
1948: Virusi hivyo vyapatikana kutoka kwenye mbu aina ya Aedes africanus msitu wa Zika
1952: Visa vya kwanza vya binadamu kuambukizwa virusi vya Zika vyaripotiwa Uganda na Tanzania
1960-80: Virusi vya Zika vyapatikana kwenye mbu na tumbili maeneo ya kati Afrika
1960-80: Virusi vya Zika vyapatikana maeneo yenye misitu na mvua nyingi Asia, ikiwemo India, Indonesia, Malaysia na Pakistan
2007: Virusi vya Zika vyaenea nje ya Afrika na Asia, kwanza katika visiwa vya Yap kwenye bahari ya pasifiki
2012: Watafiti wagundua aina mbili tofauti za virusi vya Zika, virusi vyenye asili Afrika na vingine vyenye asili Asia
Machi 2, 2015: Brazil yaripoti visa vya watu kuugua kutokana na maambukizi ya virusi vya Zika
Julai 17: Brazil yaripoti visa vya watoto kuzaliwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo
Okt. 30: Visa vya watoto kuzaliwa an vichwa vidogo Brazil vyaongezeka
Novemba 2015-Januari 2016: Visa vya Zika vyaripotiwa Suriname, Panama, El Salvador,
Mexico, Guatemala, Paraguay, Venezuela, French Guiana, Martinique, Puerto Rico,
Guyana, Ecuador, Barbados, Bolivia, Jamhuri ya Dominika, Nicaragua, Curacao,
Na Jamaica
Feb. 2, 2016: Kisa cha kwanza cha Zika kuenezwa Marekani charipotiwa, kikidaiwa kutokana sana na ngono badala ya kuumbwa na mbu.
Mei 20: WHO yatangaza kupatikana kwa
virusi vya Zika kwa mara ya kwanza Afrika kipindi cha sasa cha mlipuko,
katika visiwa vya Cape Verde. Virusi hivyo ni vya aina sawa na virusi
vilivyosababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo Brazil.
Agosti 3, 2016: Wataalamu Marekani watangaza kuanza kwa majaribio ya chanjo dhidi ya Zika.
Rais Yahya Jammeh aliyeiongoza Gambia kwa kiasi miaka 22 ametangaza
ijumaa usiku kwamba hakubaliani tena na matokeo yaliyompa ushindi
mpinzani wake Adama Barrow na kutaka uchaguzi mpya ufanyike.Jammeh
ametoa onyo kali akiwataka wagambia wabakie majumbani mwao na
kutothubutu kuingia mitaani kuandamana.Inaarifiwa wanajeshi walionekana
wakiweka vizuizi vya magunia ya mchanga katika maeneo muhimu kote kwenye
mji mkuu Banjul hali ambayo inatajwa kusababisha hali ya wasiwasi kote
katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo linaelekea kutumbukia
katika mgogoro mpya Wa kisiasa.
Uchunguzi uliofanyika kuhusiana
na matokeo ya uchaguzi wa Desemba Mosi yameonesha kutokea kwa dosari
zisizokubalika upande wa tume ya uchaguzi alisema Jammeh katika hotuba
yake iliyooneshwa kupitia Televisheni ya Taifa na kuonegeza kwamba
hatokubali tena kuachia madaraka kwa mgombea wa upinzani Adama
Barrow.Zaidi rais huyo alisema'' kama nilivyokuyakubali matokeo ya
uchaguzi kwa nia nzuri naamini kwamba tume huru ya uchaguzi ilikuwa huru
na ya kweli na ya kutegemewa,Natangaza kwamba sikubaliani na matokeo
kwa hali yoyote.
Jeshi limetawanywa katika mji mkuu huku Marekani
ikilitaka jeshi hilo kuendelea kuheshimu uatawala wa sheria na matokeo
ya urais.Tayari upinzani umejibu hatua ya rais Jammeh kwa kumkosoa na
kusema kupitia mitandao ya kijamii kwamba anakwenda kinyume na
demokrasia lakini pia upinzani umewataka wananchi wagambia wabakie
watulivu.Matokea ya hadi sasa yanaonesha Adama Barrow alishinda kwa
asilimia 43.29 ya kura wakati Jammeh akipata asilimia 39.64 na idadi
jumla ya waliojitokeza kupiga kura ni asilimia.Marekani kupitia balozi
wake mjini Banjul imetowa mwito wa Utulivu na kulitaka jeshi liendelee
kuheshimu utawala wa kisheria na matokeo ya uchaguzi wa rais.
Desemba
2 rais Jammeh alitoa hotuba iliyovuta hisia kubwa miongoni mwa wananchi
wa Gambia baada ya kukubali kushindwa na kuahidi kumpokea madaraka
mpinzani wake kwa njia ya amani tangazo ambalo lilizusha vifijo na
nderemo katika nchi hiyo.
Lakini sasa Jammeh amegeuza msimamo na
kusema kwamba uchaguzi wa Desemba Mosi ulikuwa ndio uchaguzi
uliokabiliwa na udanganyifu mkubwa kabisa kuliko chaguzi zote katika
historia ya Gambia.Nchi jirani ya Senegal imetoa tamko la kulaani
kinachoendelea Gambia huku nchi hiyo ikilitaka baraza la usalama la
Umoja wa Mataifa kukutana kulijadili suala hilo na pia kumtolea mwito
Jammeh kuyakubali matokeo na kupisha kipindi cha mpito kwa njia ya amani
na kuyakabidhi madaraka.