Taarifa kutoka ikulu imesema uteuzi wa Prof Mgaya unaanza mara moja.
Dkt Mwele Malecela, alifutwa kazi siku moja tu baada yake kutangaza kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.
Taarifa ya kufutwa kwake, iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya ikulu Gerson Msigwa, haikueleza sababu ya kufutwa kazi kwa Dkt Malecela,
Hata hivyo, kulikuwa kumetokea habari za kukinzana kutoka kwake na wizara ya afya kuhusu kuwepo kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.
Alitangaza kuwepo kwa virusi hivyo nchini Tanzania siku ya Alhamisi lakini Ijumaa, baada ya habari hizo kuenea kwenye vyombo vya habari, waziri wa afya Ummy Mwalimu akatoa taarifa kukanusha habari hizo.
Dkt Mwele Malecela alikuwa ametangaza kwamba virusi hivyo vimepatikana mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na Mkoani Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Kwa mujibu wake, virusi hivyo viligunduliwa wakati wa utafiti uliofanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.Kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti huo, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi vya Zika.
Hata hivyo wizara afya nchini humo, ilitoa taarifa ambapo inakanusha kuwepo kwa virusi hivyo.
"Kama nilivyoeleza mnamo Februari 2016, ugonjwa huu bado haujaingia nchini, na leo pia napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa Tanzania haujathibitishwa kuwepo na ugonjwa wa Zika," taarifa ya wizara ya afya imesema.
Wizara hiyo inasema uchunguzi uliofanywa na NIMR ulikuwa wa kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya.
"Matokeo haya bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina zaidi kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani," wizara ilisema.
Asili ya Zika
Jina la virusi hivyo linatokana na msitu wa Zika, Uganda ambapo virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza 1947.Wengi wa walioambukizwa aina ya awali ya virusi walikuwa wakipatwa na homa ambayo si kali sana, mwasho na maumivu katika maungio.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni