Aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa
katoliki mjini Jerusalem ambaye alipatikana na hatia ya kuwapelekea
silaha wapiganaji wa Palestina amefariki akiwa na umri wa miaka 94.
Hilarion
Capucci alihudumia kifungo cha miaka 12 jela nchini Israel kabla ya
Vatican kuingilia kati na kusaidia kumwachilia huru.
Alikuwa na historia ya uanaharakati unaohusishwa na mgogoro unaondelea mashariki ya kati.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alituma risala za rambi rambi akimtaja kuwa alikuwa mpiganiaji wa uhuru.
Vatican ilithibitisha kifo chake siku ya Jumatatu ,lakini haikusema kiini cha kifo hicho ama hata kutoa maelezo.
Capucci alizaliwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria Allepo mwaka 1922.
Alitawazwa kuwa kasisi wa kanisa la Allepo mwaka 1947 kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jerusalem.
Mwaka
1974, alikuwa akisafiri kutoka Beirut kuelekea Jerusalem ndani ya gari
lililokuwa na nambari za mwanadiplomasia wakati liliposimamishwa na
vikosi vya usalama vya Israel.
Ndani yake kulikuwa na bunduki nne
aina ya Kalashnikov, bunduki nyengine mbili aina ya pistol , silaha na
maguruneti yalionuia kupewa wanachama wa PLO.
Capucci alisisitiza
kuwa ailazimishwa kusafirisha silaha hizo ,lakini mahakama ya Israel
ilimpata na hatia ya kusafirisha silaha na kumuhukumu miaka 12 jela.
Aliachiliwa huru mwaka 1977 baada ya ombi la papa John Paul wa sita.
Capucci
alisalia katika vyombo vya habari baada ya kuachiliwa kwake , akijaribu
kuwa mpatanishi wa raia wa Marekani waliotekwa nchini Iran .
Ijapokuwa
aliwakera baadhi ya mateka wa Marekani na matamshi yake wakati
alipowatembelea ili kuangalia hali yao 1980, alihusika pakubwa katika
usafirishaji wa miili minane ya wanahewa wa Marekani waliofariki katika
jaribio la kuwaokoa wenzao.
Mwaka 1990, alisafiri hadi nchini Iraq
chini ya uongozi wa Saddam Hussein ili kusaidia kuachiliwa huru kwa
raia 68 wa Itali waliozuiliwa kuondoka nchini humo kufuatia uvamizi wa
Kuwait.
Miaka 10 baadaye Capucci aliongoza ujumbe wa viongozi wa
dini na wataalam nchini Iraq kwa umoja dhidi ya vikwazo vya Umoja wa
Mataifa.
Mwaka 2010, alikuwa ndani ya meli ya Mavi Marmara wakati
meli hiyo ya Uturuki ilioposimamishwa na makamanda wa Israel,
iliposhiriki katika usafirishaji wa misaada ili kujaribu kukiuka
kizuizi cha Ukanda wa Gaza.
Wanaharakati 10 wa Uturuki , mmoja wao
akiwa raia wa Marekani mwenye uraia wa mataifa mawili ,waliuawa na
makumi kujeruhiwa wakati ghasia zilipozuka baada ya makamanda hao
kuingia katika meli hiyo,wakishuka kutoka kamba za helikopta.
Capucchi anasema kuwa uvamizi huo haukukubalika.